Mkutano wa Afrika50 kuanza kesho Dar

DAR ES SALAAM: Serikali imesema imekamilisha maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Afrika50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika, utakaofanyika Agosti 5 hadi 6, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
–
Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 1,200 kutoka ndani na nje ya Tanzania, wakiwemo wakuu wa nchi, viongozi wa serikali, wakuu wa taasisi za fedha za kimataifa, wanahisa wa Afrika50, viongozi wa sekta binafsi, wawekezaji pamoja na washirika wa maendeleo.
–
Akizungumza leo Agosti 4, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema mkutano huo utaongozwa na Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia atawakaribisha viongozi wote watakaoshiriki.
–
Chalamila amesema miongoni mwa viongozi wa ngazi ya urais wanaotarajiwa kushiriki ni Rais wa Angola, João Gonçalves Lourenço, Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo, Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, Rais wa Kenya, William Ruto na Rais wa Gabon, Brice Clotaire Oligui Nguema.
–
Amesema mkutano huo ni miongoni mwa majukwaa makubwa barani Afrika yanayolenga kuharakisha maendeleo ya miundombinu kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, huku ukiwa pia fursa ya kuitangaza Tanzania kama kitovu cha biashara, uwekezaji na maendeleo ya miundombinu barani Afrika.
–
Kwa mujibu wa Chalamila, Serikali itatumia mkutano huo kuwasilisha miradi mbalimbali ya kimkakati kwa wawekezaji wa ndani na kimataifa, ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), Bandari ya Dar es Salaam, miradi ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme pamoja na miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kwa lengo la kuvutia uwekezaji.


