Mradi wafungua kwa fursa wafugaji maziwa

DODOMA; WAFUGAJI nchini wanatarajiwa kuongeza uzalishaji wa maziwa na kipato kupitia Mradi wa Tuzo Shindani za Watoa Huduma kwa Ajili ya Tasnia Himilivu ya Maziwa, unaolenga kuwahamasisha kutumia mbinu bora za ufugaji, malisho bora na huduma zenye tija.

Mradi huo unaotekelezwa katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Morogoro, unalenga kuongeza uzalishaji wa maziwa, kipato cha wafugaji pamoja na kuboresha huduma zinazotolewa katika tasnia hiyo.

Akizindua mradi huo unaofadhiliwa na Heifer International, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Kamani, alisema tuzo hizo ni sehemu ya jitihada za kuongeza tija katika ufugaji na uzalishaji wa maziwa kwa kuwahamasisha wafugaji kutumia teknolojia na mbinu bora za ufugaji.

Alisema Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu matumizi ya mbegu bora za malisho, uzalishaji wa malisho ya kutosha na matumizi ya teknolojia zinazoweza kuongeza uzalishaji wa mifugo.

Kamani alisema changamoto ya uzalishaji mdogo wa maziwa nchini inahitaji ushirikiano wa Serikali, wafugaji na wadau wa maendeleo ili kubadili hali hiyo na kuwawezesha wafugaji kuongeza kipato.

Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na unafikia malengo ya kuimarisha tasnia ya maziwa nchini.

Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Maziwa, George Msaja, alisema mradi huo umeanzishwa kwa lengo la kuongeza uzalishaji na masoko ya maziwa, sambamba na kuboresha huduma kwa wafugaji.

Alisema mradi huo unaofadhiliwa na mashirika mbalimbali unalenga kuwawezesha wafugaji kupata huduma bora zitakazowasaidia kuongeza uzalishaji na kupata masoko ya uhakika ya maziwa yao.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Heifer International, Mark Tsoxo, alisema kaya nyingi nchini zinategemea tasnia ya maziwa, lakini uzalishaji bado ni mdogo, jambo lililosababisha kuanzishwa kwa mfumo wa tuzo unaolenga kuchochea matokeo katika sekta hiyo.

Alisema Heifer International imeanzisha mfumo wa kulipa kwa matokeo kupitia mradi huo ili kuleta utaalamu katika utoaji wa huduma na kuhakikisha changamoto zinazowakabili wafugaji zinapatiwa ufumbuzi wa vitendo.

Muwasilishaji wa Mradi kutoka Heifer International, Edna Lusuva, alisema mahitaji ya maziwa nchini ni takribani lita bilioni 13 kwa mwaka, wakati uzalishaji uliopo ni lita bilioni 3.1, hali inayoonyesha kuwepo kwa pengo kubwa linalohitaji juhudi za makusudi.

Alisema moja ya sababu za uzalishaji kuwa mdogo ni wafugaji wengi kutumia ng’ombe wenye uwezo mdogo wa kutoa maziwa pamoja na kutotumia malisho bora.

Lusuva alisema tuzo hizo zitawahamasisha wafugaji kuongeza uzalishaji wa malisho bora na kutumia mbinu bora za ufugaji, hatua itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa na kipato.

Alisema malengo makuu ya tuzo hizo ni kuongeza uzalishaji wa maziwa, kuimarisha uhusiano kati ya watoa huduma na wafugaji pamoja na kuongeza kipato cha wafugaji wadogo.

Katika hatua nyingine, Serikali imewataka wafugaji wanaofuga katika maeneo ya mabondeni kuchukua tahadhari na kuhamishia mifugo yao katika maeneo salama kutokana na uwezekano wa mvua za El Niño kusababisha mafuriko.

Kamani alisema wafugaji wanapaswa kuchukua hatua mapema badala ya kusubiri madhara yatokee, huku akisisitiza umuhimu wa maandalizi ya malisho na maeneo salama kwa mifugo.

Kwa upande wake, NBC ilieleza kuwa wafugaji watapata fursa za kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao, huku wakihimizwa kutumia mikopo hiyo kuwekeza katika uzalishaji.

Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji Maziwa, Hamisi Mzee, alisema wafugaji wamepokea maelekezo yaliyotolewa na Serikali na wadau na watahakikisha wanayafanyia kazi ili kuongeza uzalishaji wa maziwa.

Naye Anna Almas, mzalishaji wa maziwa kutoka Mvomero, alisema wadau wa tasnia hiyo wanapaswa kutumia mradi huo kuboresha uzalishaji, malisho na huduma kwa wafugaji ili kuifanya tasnia ya maziwa kuwa na tija zaidi.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button