Msigwa: Charles Hilary kaacha somo kwa waandishi

SERIKALI imesema aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Charles Hilary ameacha fundisho kuwa uandishi wa habari na utangazaji ni utumishi unaohitaji nidhamu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema hayo wakati wa kuaga mwili wa Charles katika Viwanja vya Mapinduzi Square mjini Unguja jana.
“Charles ametufundisha kuwa uandishi wa habari na utangazaji ni utumishi, ametufundisha hata kama utafanya kazi hii kwa miaka mingi kiasi gani yeye amefanya kwa miaka zaidi ya miaka 40, lakini tuna wajibu wa kuzingatia misingi, wajibu, maadili, miongozo na nidhamu ya uandishi wa habari na sio tu kuzingatia na kuiishi,” alisema Msigwa ambaye pia ni mwandishi wa habari.
Alisema, Charles hakuona ugumu kuomba kujifunza hata kwa waliomzidi umri na alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Zanzibar alimtafuta amuelekeze baadhi ya mambo.
“Alinipigia simu akaniambia mdogo wangu nimepewa kazi niambie wapi nikufuate unipe ‘abc’, Charles ni wa 1959, mimi wa 1977 lakini anataka mimi nimpe ‘abc’ kwa sababu aliamini kwa kuwa mimi nilitangulia kumsaidia kiongozi mkubwa nitakuwa na cha kumsaidia na yote tuliyoyazungumza aliyafanyia kwa asilimia 100,” alisema Msigwa.
Alimshukuru, Rais Dk Hussein Mwinyi na viongozi wengine kwa kuendelea kuwapa nafasi waandishi wa habari kuwasaidia.
Msigwa alisema, Charles alisisitiza kufurahia kazi na kutoendekeza msongo wa mawazo na kuwa hata yeye hiyo ndiyo misingi yake katika ufanyaji kazi.
“Tusiendekeze ‘stress’ (msongo wa mawazo), mimi hiyo ndiyo misingi yangu ya kazi kuanzia kwenye familia, kazini hakuna ‘stress’, kazi ni furaha, ukiifanya kazi kwa furaha unaifanya vizuri hiyo, ndiyo ilikuwa miongozo ya Charles,” alisema.
Alisema, Charles alianza kazi ya utangazaji Radio Tanzania wakati ambao hakukuwa na vyuo vya kujifunza uandishi wa habari na walifundishwa utangazaji kwa mafunzo yaliyotolewa na redio, hivyo aliajiriwa kwa sifa ya ubora wa sauti na umahiri katika utangazaji kabla hajaenda kusoma.
Mtoto wa Charles, Faith Hilary alisema baba yake aliajiriwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) mwaka 1980 na akiwa hapo alipitia mafunzo na alifanya kazi kwenye idara mbalimbali hadi mwaka 1994.
Faith alisema baba yake alijiunga na Radio One Stereo mwaka 1994 na alifanya kazi hapo hadi mwaka mwaka 2003 alipojiunga na Shirika la Utangazaji la Ujerumani (DW) hadi mwaka 2005 alipomaliza mkataba wake na kurudi nchini.
Alisema mwaka 2006 alijiunga na Idhaa ya Kiswahili na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na alifanya kazi hadi mwaka 2015 aliporudi Tanzania na kujiunga na Kampuni ya Azam Media.
Faith alisema Desemba 2021, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alimteua Charles kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu na Februari 2023 akamteua kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hadi umauti ulipomfika.



