Mtaalamu aonya tishio magonjwa ya ini

DAR ES SALAAM; Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inapokea wastani wa wagonjwa 100 kila wiki katika kliniki ya magonjwa ya ini na mfumo wa chakula, huku zaidi ya wagonjwa 5,000 wakifuatiliwa kwa maradhi hayo, ambapo hepatitis B imeendelea kuwa tatizo kubwa.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Ini Duniani jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Ini Muhimbili, Dk Kitabu Pazi, amesema wagonjwa wengi wanaobainika kuwa na maradhi ya ini hugundulika kuwa na homa ya ini aina B (hepatitis B) , ambayo inaweza kusababisha saratani ya ini iwapo haitatibiwa mapema.
Amesema hospitali imeendesha uchunguzi na vipimo vya homa ya ini kwa wananchi pamoja na wagonjwa wanaotumia dawa za muda mrefu, ili kubaini kama dawa hizo zimeathiri ini.
“Homa ya ini B ndiyo changamoto kubwa kwa wagonjwa wetu. Wengi hawafahamu dalili zake kwa sababu ugonjwa huu unaweza kukaa mwilini kwa muda mrefu bila kuonesha dalili.
” Tunasisitiza wananchi kupima mapema na kupata chanjo ili kujikinga,” amesema Dk Pazi.
Ameongeza kuwa wagonjwa wengi wanaolazwa kutokana na maradhi ya ini husababishwa na maambukizi ya virusi vya homa ya ini aina B na C.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa Bobezi wa Magonjwa ya Ini kutoka Kitengo cha Magonjwa ya Ini na Mfumo wa Chakula cha MNH-Mloganzila, Dk Tuzo Lyuu, amesema homa ya ini husababishwa na virusi vya aina tano: A, B, C, D na E.
Amefafanua kuwa virusi vya hepatitis A na E huenezwa kupitia chakula na maji yasiyo salama, huku aina B, C na D zikiambukizwa kupitia damu, kujamiiana na kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto.
“Njia bora za kujikinga ni kuhakikisha usafi wa chakula na maji, kutumia damu salama wakati wa kuongezewa damu, kufanya vipimo mapema na kupata chanjo dhidi ya homa ya ini aina B,” amesema Dk Lyuu.



