MTOTO Elina Amos, mwenye umri wa miaka minne, mkazi wa mtaa wa Barenge, Geita amefariki dunia baada ya kutumbukia katika kisima kirefu kilichopo mtaa huo wakati akipita.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, Insipekta Edward Lukuba, amethibitisha tukio hilo na kueleza limetokea leo Januari 13, 2023, saa nne asubuhi, ambapo mtoto huyo alikuwa ameagizwa na wazazi wake na wakati akipita uchochoroni akatumbukia kwenye kisima hicho.
“Alitumbukia kwenye kisima ambacho kipo kwenye uchochoro wa huo mtaa wa Barenge karibia na msikitini, (msikiti wa Ijumaa Geita), hiki kisima kilikuwa hakina mfuniko.
“Rai ambayo tumeendelea kuitoa, visima vyote vijengewe msingi, lakini pia viwekewe mfuniko, kwani kisima hiki kilikuwa wazi kikasababisha mtoto ambaye alikuwa anapita kuzama na kufariki,” amesema.
Amesema uwepo wa visima holela ndani ya mji wa Geita ni changamoto kubwa, inayosababisha matukio ya aina hiyo, kwani ndani ya mwaka 2022, pekee takribani watu 25 walifariki kwa kuzama maji.