Nduli yaamka: Viongozi wafundwa kutetea haki na kukemea ukatili

IRINGA: Katika hatua ya kuijenga jamii inayozingatia haki, amani na utawala wa sheria, viongozi wa Kata ya Nduli, mjini Iringa wamepewa mafunzo maalum ya utawala bora na namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na kijamii, kupitia semina iliyojaa maarifa, hoja nzito na vionjo vya maamuzi ya kishujaa kwa maendeleo ya jamii.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Idara ya Sheria ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) – Kanda ya Iringa, Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia, na wataalamu wa ustawi wa jamii, yakiwa na lengo la kuwanoa viongozi wa vijiji na mitaa kuwa walinzi wa sheria na haki kwa vitendo.
Mwenyekiti wa TLS Kanda ya Iringa, Wakili Moses Ambindwile, alitumia jukwaa hilo kuwakumbusha viongozi kuwa nguzo ya utawala bora si jambo la hiari bali ni wajibu wa kisheria na maadili ya uongozi.
“Ukikanyaga misingi ya utawala bora, unakaribisha migogoro, hofu, na chuki kwa wananchi. Tunataka viongozi wa Nduli waongoze kwa mfano na kwa kufuata sheria kila hatua,” alisema kwa msisitizo.
Aliongeza kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa wakijichukulia mamlaka ya kimahakama bila uhalali, jambo ambalo ni kosa la kisheria.
“Mtendaji au mwenyekiti hana mamlaka ya kukamata au kuamuru mali ya mwananchi ishikwe bila ridhaa ya mahakama. Sheria ni msumeno, inakata kote,” alieleza kwa mfano ulioibua mjadala mkali miongoni mwa viongozi waliokuwepo.
Katika tukio hilo pia, mjadala mkali uliibuka kuhusu wajibu wa wanandoa kwenye ndoa zao, ambapo Wakili Ambindwile alifafanua kwa kina kuwa Sheria ya Ndoa inawataka wanandoa kutimiza majukumu ya kindoa ikiwemo unyumba.
“Kukataa kutimiza wajibu huo ni sababu ya msingi kuvunja ndoa kisheria. Tusifanye ndoa kuwa jela ya kihisia,” alifafanua, kauli iliyowafanya baadhi ya washiriki kuhema kwa mshangao.
Inspekta Loveness Maingu kutoka Dawati la Jinsia aliwasha moto wa mijadala aliposema:
“Ukatili hauna jinsia. Hata wanaume wanateseka kimya kimya. Tunawahimiza wote – wakubwa kwa wadogo – wasikae kimya, waseme, ili tusaidie.”
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii, Renatus Mwageni, alisisitiza umuhimu wa wazazi kuwa makini na mienendo ya watoto wao, akieleza kwamba watoto wanaopitia ukatili huonyesha dalili ambazo wazazi wanapaswa kuzitambua mapema.
“Kilio kisicho na sababu, kujitenga au hofu zisizoelezeka ni alama tosha za kuomba msaada wa haraka. Tuchukue hatua kabla maumivu hayajageuka majuto,” alisema kwa hisia.
Semina hii ni mwendelezo wa mikakati ya Halmashauri ya Iringa kuweka msingi imara wa jamii yenye haki, heshima na usawa, kupitia uelewa wa kisheria na ushirikiano wa karibu na vyombo vya sheria na jamii.
Nduli sasa si tu jina la kata – bali ni alama ya mabadiliko ya kiuongozi na ulinzi wa utu wa binadamu, alisema diwani wa kata hiyo Bashir Mtove.