Programu ya ‘Kopa Ng’ombe, Lipa Maziwa’ kuwaokoa wafugaji Kagera

KAGERA: Maelfu ya wafugaji katika mikoa ya Kagera wanatarajiwa kunufaika na programu ya iMbeju Kilimo Kopa Ng’ombe, Lipa Maziwa, inayolenga kuongeza uzalishaji wa maziwa, kipato na kuwawezesha wafugaji wadogo kujenga biashara endelevu ya mifugo.

Programu hiyo imezinduliwa na CRDB Foundation kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ikiwa na lengo la kuwawezesha wafugaji kuondokana na utegemezi wa mazao ya msimu mmoja na kujikita katika uzalishaji wa maziwa, ambayo yanaweza kuwa chanzo cha kipato cha kila siku kwa familia.

Programu hiyo imeanza rasmi katika wilaya za Kyerwa, Karagwe na Missenyi, mkoani Kagera, ambapo wafugaji wamewezeshwa kupata jumla ya ng’ombe 1,077 kwa awamu moja kupitia mfumo wa mikopo.

Akizindua programu hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Bashiru Ally Kakurwa, amesema amevutiwa na namna sekta binafsi na Serikali zinavyoweza kushirikiana kubuni programu zinazolenga kumuinua mfugaji mdogo kwa kuongeza uzalishaji, kipato na uwezo wa kuwekeza.

Amesema mpango huo unapaswa kuleta manufaa kwa mnyororo mzima wa thamani, ikiwemo wafugaji kupata kipato kupitia maziwa na mbolea, familia kunufaika na lishe bora, huku viwanda vya ndani vikipata malighafi ya kutosha.

Dkt. Bashiru amesema programu hiyo inapaswa kuleta matokeo yanayopimika, hususan katika kuongeza uzalishaji wa maziwa na kipato cha mfugaji.

Pia amesisitiza umuhimu wa kusimamia vizuri mfumo wa bima za mifugo, akieleza kuwa wafugaji wanapolipia bima wanapaswa kupata huduma na msaada stahiki pale mifugo yao inapokumbwa na changamoto.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation, Tuli Mwambapa, amesema programu hiyo inalenga kumtoa mfugaji kutoka katika uzalishaji mdogo na kumjenga kuwa mjasiriamali kupitia upatikanaji wa maarifa, teknolojia, mitaji, huduma za kifedha na masoko.

Amesema mpango huo haujikita katika kumpatia mfugaji fedha pekee, bali unalenga kujenga biashara ya mifugo yenye uwezo wa kukua na kutoa kipato endelevu.

Kwa mujibu wa Mwambapa, mfugaji mdogo anaweza kuomba mkopo wa ng’ombe mmoja hadi 10 kulingana na uwezo na mahitaji yake.

Amesema hadi wakati wa kuzinduliwa kwa programu hiyo, tayari wamepokea maombi kutoka kwa wafugaji takribani 5,000 katika wilaya za Karagwe, Kyerwa na Missenyi.

Ameeleza kuwa katika mfumo huo, mfugaji atarejesha mkopo kupitia maziwa atakayozalisha, ambapo asilimia 60 ya thamani ya maziwa itatumika katika marejesho ya mkopo huku asilimia 40 akipewa fedha taslimu.

Amesema baada ya kumaliza marejesho ya mkopo, mfugaji ataanza kupata asilimia 100 ya fedha kutokana na maziwa yake na atapewa fursa ya kuomba mkopo mwingine wa mifugo.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Maziwa cha Kahama Fresh, Josam Ntangeki, amesema katika mfumo huo marejesho ya mkopo yatafanyika kupitia maziwa yatakayozalishwa na ng’ombe waliotolewa kwa wafugaji.

Amesema mitamba iliyotolewa kwa wafugaji ina mimba, jambo ambalo litasaidia kuongeza mifugo na uzalishaji wa maziwa, huku akieleza kuwa mfugaji anaweza kumaliza marejesho ya mkopo ndani ya kipindi cha miaka mitatu na hatimaye kumiliki mifugo hiyo moja kwa moja.

Mratibu wa mpango huo mkoani Kagera ambaye pia ni Mkurugenzi wa CADRESS, Leonard Kachebonaho, amesema imechukua takribani miaka minane kuchakata wazo hilo hadi kulifikisha kwa wakulima na wafugaji.

Amesema awali changamoto kubwa ilikuwa ni kutokuwa na uhakika wa soko la maziwa, lakini baada ya kuanzishwa kwa kiwanda cha maziwa, mazingira ya biashara yamebadilika na sasa kuna fursa ya kuwasaidia wafugaji kuongeza uzalishaji.

“Tumekuwa tukiona mazao mengi yakitegemea msimu, lakini maziwa ni bidhaa inayozalishwa kwa kipindi chote na inaweza kumsaidia mfugaji kukabiliana na mahitaji ya kila siku,” amesema.

Wadau kutoka sekta binafsi walioshiriki katika uzinduzi wa programu hiyo wameiomba Serikali kuwahimiza maafisa ugani katika halmashauri kuhakikisha wanatumia nafasi zao kutoa huduma za ugani kwa wafugaji, pamoja na kutoa msaada wa haraka pale changamoto zinapojitokeza.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button