MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima, ameitaka Kampuni ya M/S Sogea Satom kukamilisha kwa wakati mradi wa maji Butimba, ili kuongeza wigo wa huduma kwa wananchi.
Alitoa wito huo hivi karibuni katika ziara yake ya kutembela miradi mbalimbali, akaeleza kufurahishwa na maendeleo ya mradi huo wa Butimba.
“Tunahitaji mradi huu ukikamilika wanufaika wote waunganishwe na huduma. Nawaagiza wakuu wote wa wilaya kulizingatia hili,” alisema.
Mradi huo unasimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa mazingira Mwanza (Mwauwasa) na kujengwa kwa gharama ya Sh bilioni 69.
Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Leonard Msenyele, alisema: “ Mradi ni mkubwa, wa kisasa na umegawanyika katika maeneo kadhaa ikiwemo tangi kubwa, eneo la kuondoa madini tofauti, kubadilisha tabia ya maji, kuchuja maji, kuondoa matope, kuuwa wadudu na usafirishaji maji.”
Alisema mradi huo ulianza kutekelezwa Februari Mosi 2021 na unatarajiwa kukamilika Februari mwaka kesho, akaahidi usimamizi imara ambao utafanya mradi kukamilika kwa muda uliopangwa.
“Mradi huu wa ujenzi wa chanzo hiki kipya cha Butimba utakapokamilika kwa awamu hii ya kwanza utazalisha lita 48,000 kwa siku. Wakazi 450,000 wa Kata za Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Lwamina, Fumagila, Sawha, Igoma, Kishiri na Nyamanoro watanufaika,” alisema.
Kwa mujibu wa Msenyele, wakazi wengine watakaonufaika ni wa Wilaya ya Misungwi maeneo ya Usagara, Nyashishi na Fella pamoja na Wilaya ya Magu maeneo ya Kisesa, Bujora na Isangijo.