RC Katavi kuunda tume mgogoro TAWA, wananchi

RC Katavi kuunda tume mgogoro TAWA, wananchi

MKUU wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amewaahidi wananchi wa Kata ya Kamsisi wilayani Mlele kuwa, ataunda tume ya wataalamu itakayochunguza eneo lenye mgogoro kati ya wananchi na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), lenye ukubwa wa ekari 131.

RC Mrindoko ametoa ahadi hiyo, wakati wa mkutano wa hadhara katika ziara yake wilayani humo, kuwa ndani ya siku kumi tume itakuwa imeundwa, hiyo ikiwa ni baada ya wananchi kumuomba warejeshewe eneo hilo, kwa kuwa wamekuwa wakilitumia kwa muda mrefu kwa uzalishaji wa chakula.

Amesema kamati hiyo itaundwa na pande zote mbili kati ya wataalamu kutoka ofisi yake na wawakilishi kutoka upande wa wananchi, kwa kile alichosema mgogoro huo unahitaji busara za pande zote mbili, kwani zote zina makosa.

Advertisement

Hata hivyo, TAWA wameanza kujenga ofisi zake katika eneo hilo linalopakana na hifadhi, huku wananchi wakigoma kupelekwa eneo linguine, ambalo wanadai sio zuri kwa uzalishaji wa chakula, hivyo wanataka wasalie eneo hilo.