Ruvuma wazindua Mradi kuboresha elimu msingi

RUVUMA; Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Wakili Mary Makondo, amezindua mradi wa MsingiTek unaolenga kujenga stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la tatu.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika Shule ya Msingi Humbaro, Kijiji cha Mpitimbi B, Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Makondo amesema, teknolojia ya kidijitali imeleta mageuzi makubwa katika elimu ya msingi kwa kusaidia watoto kushinda changamoto za kujifunza.

Ameeleza kuwa kila mwanafunzi anatumia kishikwambi (tablet) kinachofanya kazi bila mtandao, huku ushiriki wao ukifuatiliwa na maendeleo yao yakipimwa kwa zana za kitafiti.

Amewaagiza walimu na viongozi wa shule kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa, ili viweze kudumu kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu Mkoa wa Ruvuma, Mwalimu Edith Mpinzile, alisema, bado mkoa unakabiliwa na changamoto ya wanafunzi kufika darasa la tatu bila kumudu stadi za KKK.

Alisema, tatizo hilo linachochewa na utoro wa wanafunzi, hali inayowafanya kukosa mwendelezo wa masomo.

Kwa mujibu wa Mpinzile, mradi wa MsingiTek umeleta mbinu mpya za ufundishaji wa kidijitali ambazo si tu zinarahisisha ufundishaji, bali pia zinawavutia wanafunzi kuhudhuria shule kwa wingi.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Fedha wa shirika la Imagine Worldwide, Deo Chuwa, alisema,mradi wa. MsingiTek kwa sasa unatekelezwa katika halmashauri tatu za Mkoa wa Ruvuma ambazo ni Songea DC, Mbinga DC na Tunduru.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button