Samia asema hakuna upungufu wa chakula

Rais Samia Suluhu Hassan

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema bado Tanzania ina chakula cha kutosha na hakuna tishio la kuwa na uhaba.

Rais Samia alibainisha hayo jana katika uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam wakati akishiriki Jubilei ya miaka 50 ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA)

Alisema kwenye ghala la hifadhi ya taifa la chakula kuna takribani tani 150,000 kwa ajili ya kutumiwa endapo kutatokea wakati mgumu wa upungufu wa chakula.

Advertisement

Rais Samia alisema hayo akijibu ombi la Mwenyekiti wa Wawata, Evelyn Mtenga kuhusu mikakati ya kudhibiti tatizo la njaa nchini kutokana na kuwepo kwa dalili za upungufu wa chakula.

Mtenga alisema takwimu zinaonesha dalili ya kutokuwepo chakula cha kutosha mwaka huu hadi msimu ujao kutokana na mavuno hafifu.

“Tunatambua linapotokea baa la njaa wanaoathirika zaidi ni wanawake na watoto. Tunaomba serikali iweke mikakati madhubuti ya kuwezesha kuwepo kwa chakula cha kutosha,” alisema.

Rais Samia alisema, “Mmeliona hili vizuri kwa sababu miaka michache ijayo dunia inaangalia suala la kutokuwa na chakula cha kutosha. Kuna nchi ambazo leo tayari wameshaingia kwenye janga hili na nyingine bado,”

Aliongeza“Nataka niwahakikishie Tanzania bado tuko katika hali nzuri pamoja na mavuno hafifu kwa msimu uliopita, ghalani kuna tani zisizopongua 150,000 tumeziweka kwa ajili ya wakati mgumu,” alisisitiza rais Samia.

Alisema mwaka  2019/20 ghala hilo ilikuwa na hifadhi ya tani 50,000 na nchi ilipoingia katika wakati mgumu zilisaidia Watanzania na nchi jirani lakini kwa sasa ghala hilo limeongezewa uwezo wa hifadhi kwa zaidi ya mara tatu.

“Tuendelee kumuomba Mungu atushushie mvua zenye neema na baraka ili tuendelee kuvuna. Serikali inajitahidi kutoa ruzuku kwa wakulima ili wahimili bei za pembejeo na walime maeneo makubwa na kuvuna zaidi. Nawahakikishia kwamba mpaka sasa Tanzania haijaingia kwenye orodha ya nchi zitakazokuwa na njaa hivi karibuni,” alisema.