Serera ataka usimamizi bora ushirika
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayeshughulikia mambo ya ushirika na umwagiliaji, Suleiman Serera amewataka wadau wa zao la korosho kusimamia kwa ukaribu sekta ya ushirika ili uwekezaji unaofanywa na serikali kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi uweze kufanywa na vyama vya ushirika
Akizungumza leo mkoani Mtwara wakati wa kikao cha utendaji kuhusu kujadili mfumo wa ununuzi wa korosho na utaratibu wa minada kwa simu wa mwaka 2024/2025, Naibu Katibu Mkuu huyo amesema wanapozungumzia suala la ushirika ni watu na siyo viongozi wanaoonekana katika chama.
Kikao hicho kimefanyika katika manispaa ya mtwara mikindini mkoani humo na kukutanisha wadau wa korosho kutoka mikoa minne inayolima zao hilo nchini ikiwemo Mtwara, Lindi, Ruvuma pamoja na Pwani.
‘’Ili ushirika uonekanane kuna mnyororo mrefu sana wa watu wanakuwepo wakiwemo wauzaji, wanunuzi, watu wanosimamia sera hivyo hao wote wanaposhirikiana ndiyo tunaona huo ushirika‘’amesema Serera.
Amesema hata kama wanao wananunuzi ambao watanunua na mambo mengine lakini wanatakiwa wafanye vitu vingine Kupitia ushirika kwani dhamira ya serikali ni kurudisha hadhi ya ushirika hususani wa mazao na uendeshwe kisasa.
Pia uwekezaji ufanywe kitaalam na ukiwa na lengo la kumnufaisha mwana ushirika moja kwa moja ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa wakati malipo ya wakulma wa zao hilo, suala la minada na mengine.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Francis Alfred ametoa taarifa kuhusu kuanza kwa minada ya korosho msimu huo wa mwaka 2024/2025 ambayo ni Oktoba 11, 2024.
Pia ameomba kama kuna mdau yoyote mwenye mashaka na tarehe hiyo au ana mawazo tofauti washirikishane.
Hata hivyo amevisisitiza vyama vikuu ya ushirika nchini katika zao hilo kuweka alama kwenye magunia ya korosho kuweza ili kuwadhibiti wale wote wanaonunua korosho kinyume na taratibu.
Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Nchini (TCDC) Dk. Benson Ndiege amesema watahakikisha wanatoa ushirikiano kwa taasisi zote katika kazi hiyo ya mnada ya korosho inayotarajiwa kuanza hivi karibuni katika maeneo mbalimbali inayolima zao hilo.
Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) Asangye Bangu amesema bodi hiyo imekuwa ikipokea changamoto mbalimbali zinazotokana na waendesha maghala wenyewe.
Pia wanunuzi, vyama vikuu vya ushirika na Cbt hivyo wamewasilisha mapendekezo ambayo tayari yameshafanyiwa kazi na mengi wameshawasiliana na wadau ili kuhakikisha jambo hilo linakwenda vizuri zaidi.