SERIKALI imesema itachukua hatua kali za kisheria kwa wasimamizi wa makundi ya mitandao ya kijamii na watu binafsi watakaosambaza maudhui yenye viashiria vya ushoga na usagaji.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema Jumapili mkoani Dar es Salaam kuwa, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imebaini kuwa baadhi ya watazamaji wa maudhui ya kulipia mtandaoni wamekuwa wakitazama na kusambaza maudhui hayo zikiwemo video kwenye mitandao ya kijamii.
Nape aliwaeleza waandishi wa habari kuwa uwepo wa huduma hizo zinazopatikana ulimwenguni zinawafanya watu kupokea tamaduni, mila na desturi kupitia picha jongefu wanazoangalia mtandaoni baada ya kulipia.
Alisema ni kosa kisheria kwa mtu yeyote kusambaza maudhui hayo hata kama yanalenga kuelimisha, badala yake wanapotumiwa video hizo wafute na si kuzisambaza.
“Sheria na kanuni zinazoshughulikia maudhui zipo na tunafanya uchambuzi kuwapata wanaosambaza video hizi. Niwahakikishie tutakapoanza kuwazoa jamii isipate taharuki kwani tutatenda haki kwa kuwapeleka kwenye vyombo husika na adhabu zake ni kali…ukitumiwa futa, delete kabisa,” alisema Nape.
Alisema baada ya kufuatilia vyombo vyote vya utangazaji vilivyopewa leseni ya kurusha maudhui nchini, wamebaini havijatenda makosa hayo na kuwa wataendelea kuvifuatilia kuhakikisha maudhui hayo hayarushwi.
Nape alisema utandawazi kupitia mitandao ya kijamii umefanya utengenezaji, uandaaji na usambazaji wa maudhui usiwe na mipaka na kwamba wameshindwa kudhibiti kila kitu kinachowekwa mtandaoni kwa sababu zipo video zinazorushwa mitandaoni zikitoka nje ya nchi na kutumwa kwa Watanzania.
“Kiujumla anga letu la mtandao liko salama kwani TCRA wapo kazini kuhakikisha kuwa tunaendelea kuwa salama na hata inapotokea kuna maudhui hasi na yanayokiuka sheria, inachukua hatua stahiki kwa wanaohusika kwa kushirikiana na vyombo vya dola hasa jeshi la polisi,” alisema.
Nape alisema wazazi, walimu na walezi wana wajibu wa kuwalinda watoto kutokana na maudhui yasiyofaa hasa yanayorushwa kwenye mitandao ya kijamii.
Alisema serikali itaendelea kuweka mkazo kuhamasisha utengenezaji wa maudhui ya ndani yenye ubora na yanayozingatia utamaduni, mila, desturi na maadili ya Mtanzania.