Serikali yapongeza elimu ya vipimo kwa watoto

DODOMA: NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Londo, amepongeza Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kwa mpango wake wa kuwajengea watoto uelewa wa vipimo, akisema hatua hiyo imezaa mabalozi wanaoweza kueneza elimu hiyo kwa jamii.

Londo alitoa pongezi hizo baada ya kupokea elimu kuhusu umuhimu wa kutumia vipimo sahihi kutoka kwa wanafunzi wa Klabu ya Vipimo (Vipimo Club) ya Shule ya Msingi Mtemi Mazengo jijini Dodoma, waliokuwa wakitoa elimu kwa wananchi katika banda la WMA kwenye Maonesho ya 33 ya Wakulima Nane Nane yanayoendelea jijini hapa.

Londo alishangazwa na ufasaha na uelewa wa wanafunzi hao, ambao walimweleza kwa kina umuhimu wa kutumia vipimo sahihi, kuandika taarifa kwa usahihi kwenye vifungashio vya bidhaa pamoja na madhara ya vitendo vya lumbesa.

“Nimefurahishwa sana. Watoto hawa ni mabalozi wazuri wa jamii. Uwekezaji wa WMA katika kizazi kijacho unaleta matokeo, hongereni sana,” alisema Londo.

Alisema hatua ya kuwapatia watoto elimu ya vipimo tangu wakiwa shuleni ni muhimu katika kujenga kizazi kinachofahamu haki na wajibu wa mtumiaji na mfanyabiashara katika matumizi ya vipimo, hivyo kusaidia kupunguza malalamiko na migogoro inayotokana na vipimo visivyo sahihi.

Wanafunzi hao walishiriki katika ziara iliyoratibiwa na WMA ikiwa ni sehemu ya mpango wa kutoa elimu ya vipimo kwa vitendo, ambapo badala ya kuwa wasikilizaji pekee, waligeuka kuwa watoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda hilo.

Kupitia mpango huo, WMA inalenga kuwajengea wanafunzi uelewa wa vipimo kwa nadharia na vitendo ili wawe mabalozi wa elimu hiyo katika familia na jamii zao.

Katika maonesho hayo, wanafunzi hao walitoa huduma mbalimbali katika banda la WMA, zikiwemo kutoa elimu, kuonyesha matumizi ya aina mbalimbali za vipimo na kujibu maswali ya wananchi kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi katika biashara na matumizi ya kila siku.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa WMA, Francis Olwero, alisema wakala huo umejipanga kuendeleza Klabu za Vipimo katika shule mbalimbali ili kuwajengea wanafunzi uelewa mpana wa masuala ya vipimo na kutumia kundi hilo kama mabalozi wa kusambaza elimu nchini.

Alisema ushiriki wa wanafunzi hao katika maonesho hayo umedhihirisha kuwa mbinu ya kuwapa elimu ya vipimo kwa nadharia na vitendo ina tija, kutokana na uwezo waliouonesha wa kueleza masuala hayo kwa wananchi.

“Wanafunzi hawa wameonesha wazi kwamba mbinu hii ina tija. Tunataka kuendelea kuwajengea uwezo ili wawe mabalozi wa elimu ya vipimo katika jamii zao,” alisema Olwero.

Kiongozi wa Klabu ya Vipimo kutoka Shule ya Msingi Mtemi Mazengo, Glory Enock, aliishukuru WMA kwa kuanzisha klabu hiyo na kuwapatia wanafunzi elimu ya vipimo, akisema maarifa hayo yamewasaidia kufahamu haki za watumiaji na umuhimu wa matumizi sahihi ya vipimo.

Alisema ziara yao katika Maonesho ya Nane Nane imelenga pia kujenga utamaduni wa “Pima kwa Haki, Pata Faida Halali”, huku wakitumia maarifa waliyopata kuwaelimisha wazazi, wafanyabiashara na wananchi wengine.
“Tumefundishwa, sasa tunafundisha wazazi na wafanyabiashara kutumia mizani sahihi,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button