Serikali yatoa maelekezo kuadimika kwa saruji

DODOMA; Serikali imewapa siku saba wamiliki wa viwanda vya kuzalisha saruji nchini kuwasilisha mapendekezo ya namna ya kutatua changamoto ya bei ya saruji inayotajwa kuwa juu katika soko pamoja na upatikanaji wake.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Salum, kukutana na kufanya mazungumzo na wamiliki wa viwanda vya saruji Agosti 18, 2026 jijini Dodoma.
Salum amesema, kikao kimelenga kutafuta suluhu ya changamoto iliyosababisha kuadimika kwa bidhaa hiyo na bei kuwa juu sokoni.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na viongozi wa taasisi mbalimbali zinazohusika na udhibiti, viwango na masoko, ikiwemo Tume ya Ushindani (FCC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), TanTrade, pamoja na Wakurugenzi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Salum amesisitiza umuhimu wa kupata suluhu ya kudumu itakayosaidia kuhakikisha saruji inapatikana kwa bei inayozingatia maslahi ya wazalishaji, wafanyabiashara na wananchi.
“Serikali imewataka wazalishaji kutumia muda huo wa siku saba kufanya tathmini ya changamoto zinazoathiri bei ya saruji na upatikanaji wake sokoni na kuwasilisha mapendekezo yanayoweza kusaidia kupunguza au kudhibiti ongezeko la bei ya bidhaa hiyo na upatikanaji wake.”amesema Balozi Salum
Hatua hiyo inatajwa kuwa sehemu ya jitihada za Serikali za kuhakikisha mazingira ya biashara yanakuwa rafiki huku wananchi wakipata bidhaa muhimu kwa bei inayokubalika.

Kikao hicho pia kimeweka pamoja wadau muhimu wa sekta ya saruji ili kujadili kwa pamoja masuala yanayohusu uzalishaji, ushindani, viwango na upatikanaji wa bidhaa hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.
Baada ya siku saba, Serikali inatarajiwa kupitia mapendekezo yatakayowasilishwa na wazalishaji na kuendelea na hatua zinazolenga kupata suluhu ya changamoto ya upatikanaji pamoja na bei ya saruji nchini.



