Serikali yazidi kusogeza karibu huduma za afya

BARIADI, Serikali imeendelea kusogeza karibu huduma za afya  kwa wananchi, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Zahanati ya Bipyayi  kuzinduliwa rasmi kwa ajili ya kutoa huduma.

Kukamilika kwa zahanati hiyo kutafanya wananchi wa Kijiji cha Bipyayi, Kata ya Nyangokolwa, Halmashauri ya Bariadi, mkoani Simiyu, wasiende tena umbali mrefu kutafuta huduma za afya . Zahanati hiyo ilizinduliwa jana na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa.

Akisoma taarifa ya mradi huo mara baada ya Mwenge wa Uhuru kuwasili kwa ajili ya uzinduzi, Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Habab Habab, alisema awali wananchi wa eneo hilo walikuwa wakienda umbali mrefu wa karibu kilometa 10 kufuata huduma za afya na kwamba tayari serikali imetoa vifaa vyote muhimu ili huduma zianze kutolewa mara moja.

Habab alibainisha kuwa katika ujenzi wa mradi huo, wananchi walichangia kiasi cha Sh milioni 19.4. Serikali Kuu ilitoa Sh milioni 50, huku halmashauri ikitoa Sh milioni 50 nyingine kutoka kwenye mapato ya ndani.

“Ujenzi wa zahanati hii ulianzishwa na wananchi wenyewe baada ya kuona tunateseka sana kwenda Mtaa wa Nyangokolwa kutafuta huduma. Leo ujenzi umekamilika. Tunashukuru sana serikali,” alisema Habab.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button