Sheria ya ndoa inavyokwamisha ndoto za wasichana

DAR ES SALAAM; ASUBUHI moja mwaka 2020, Monica Msuta alibeba ndoo kana kwamba anaelekea kuchota maji kama ilivyokuwa kawaida, lakini siku hiyo haikuwa ya kawaida. Ndani ya moyo wake alikuwa amefanya uamuzi ambao ungeamua mustakabali wa maisha yake.
Badala ya kwenda kisimani, alianza safari ya kukimbia ndoa. Akiwa na miaka 13, Monica alikuwa tayari amepoteza wazazi wake kwa ajali. Badala ya kupata faraja na ulinzi kutoka kwa ndugu, alijikuta akikabiliwa na shinikizo la kuolewa na mwanaume mtu mzima, aliyekuwa rafiki wa baba yake mdogo.
“Ndoto yangu ilikuwa kusoma. Nilipoambiwa niolewe nilijua nikikubali, ndoto zangu zingekufa,” anasema.
Wakati watoto wengi wa umri wake walikuwa wakijiandaa kuanza kidato cha kwanza, Monica alikuwa akipambana kuokoa haki yake ya msingi ya kupata elimu.
Baada ya kuona baba yake mdogo hakuwa tayari kusikiliza kilio chake, aliamua kutoroka kutoka Kijiji cha Mbwewe, Pwani. Kwa siri aliwasiliana na dada yake aliyekuwa akiishi Dar es Salaam kupitia simu ya jirani.
Dada yake alimtumia nauli na asubuhi iliyofuata Monica aliondoka nyumbani bila kuaga, akijua kuwa kubaki kungeweza kumaanisha kuolewa kinyume na mapenzi yake.
“Niliamini Mungu alikuwa ananilinda. Nilijua nikivumilia nitafika nilikokuwa nataka kwenda,” anasema.
Hatimaye alifika Dar es Salaam na kuanza maisha mapya akiwa na dada yake. Ingawa dada huyo alikuwa akijitafutia riziki kupitia biashara ndogo, hakukubali mdogo wake aachane na ndoto ya elimu.
Alimtafutia shule na kumtia moyo kuendelea kusoma.

Leo Monica yuko kidato cha nne katika Shule ya Vijaliwa Vingi na anatarajia kufanya mtihani wa kuhitimu Oktoba mwaka huu. Anaonesha uwezo mkubwa, hasa katika somo la Jiografia, huku walimu wake wakimtia moyo, kumpatia vitabu na kumwelekeza namna ya kujisomea.
“Ninasoma kwa bidii kwa sababu nilijua elimu ndiyo ingeweza kubadili maisha yangu,” anasema.
Dada yake Monica anasema ameamua kuhakikisha mdogo wake anafanikiwa kwa kuwa hataki akumbane na changamoto alizopitia yeye.
“Ingawa mimi ni dada kwake, lakini pia nimesimama kama baba na mama kuhakikisha anapata haki yake ya elimu,” anasema.
Simulizi ya Monica si ya msichana mmoja pekee. Ni taswira ya maelfu ya watoto wa kike nchini wanaokabiliwa na shinikizo la kuolewa kabla ya kutimiza ndoto zao.

Kwa mujibu wa takwimu za (Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) zinazotokana na tafiti za kitaifa, takribani asilimia 29 ya wasichana Tanzania huolewa au kuingia katika muungano kabla ya kutimiza miaka 18, sawa na karibu msichana mmoja kati ya watatu. Aidha, zaidi ya wasichana na wanawake milioni 6.6 nchini wameolewa wakiwa watoto.
Hali hiyo imeibua mjadala mpana kuhusu ulinzi wa watoto wa kike, hasa kutokana na tofauti iliyopo kati ya Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inayomtambua mtoto kuwa mtu mwenye umri chini ya miaka 18 na Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 yenye vifungu vinavyoruhusu mtoto wa kike kuolewa chini ya umri huo katika mazingira yaliyowekwa na sheria.
Kwa miaka mingi, wanaharakati wa haki za wanawake na watoto wamekuwa wakieleza kuwa hali hiyo imechangia kuendeleza ndoa za utotoni na kuwanyima wasichana fursa ya elimu, afya na maendeleo.
Mwaka 2019, Mahakama ya Rufaa ilithibitisha uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi iliyofunguliwa na mwanaharakati Rebecca Gyumi, ikieleza kuwa vifungu vinavyoruhusu ndoa za watoto vina ubaguzi na vinapaswa kurekebishwa ili umri wa chini wa kuoa na kuolewa uwe miaka 18 kwa wote.
Hata hivyo, mchakato wa marekebisho hayo bado haujakamilika.
Gyumi anasema kuchelewa kwa mabadiliko hayo kunawaacha watoto wengi wa kike katika mazingira hatarishi.
“Mahakama ilishatoa maelekezo tangu mwaka 2019, lakini bado sheria haijabadilishwa. Kila mwaka unaopita kuna watoto wanaopoteza haki yao ya elimu na ndoto zao,” anasema.
Anasema kutokuwepo kwa mwafaka wa haraka miongoni mwa wadau kunaendelea kuwaumiza watoto wanaosubiri kulindwa na sheria.
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dk Rose Reuben anasema Sheria ya Ndoa imeendelea kuwa kikwazo kwa maendeleo ya watoto wa kike.
Anaeleza kuwa wakati sheria ya elimu inalinda wanafunzi dhidi ya ndoa na ujauzito, watoto wa kike ambao hawapo shuleni wanaweza kubaki katika mazingira yanayowafanya kuwa katika hatari ya kuozeshwa.
“Hii ina maana mtoto anayesoma analindwa, lakini ambaye hayupo shuleni anaweza kuachwa kwenye mazingira yanayochochea ndoa za utotoni. Mtoto ni mtoto, bila kujali kama yuko darasani au la,” anasema.
Kwa mujibu wa Dk Rose, baadhi ya familia maskini bado huona ndoa kama njia ya kupata mali kupitia mahari, jambo linalowanyima wasichana nafasi ya kuendelea na masomo.
Anasisitiza kuwa kumuelimisha mtoto wa kike kuna manufaa ya muda mrefu kwa familia na taifa kuliko faida ya muda mfupi inayopatikana kupitia mahari.
Viongozi wa kidini, kimila wataka mabadiliko
Pamoja na mwito wa kurekebisha sheria, baadhi ya wadau wanaeleza kuwa mchakato huo unahitaji ushirikishwaji mpana kutokana na kugusa masuala ya mila, dini na desturi.
Mbunge wa Lupembe na mwanasheria, Edwin Swalle anasema Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 iliandaliwa kwa kuzingatia makundi mbalimbali ya kijamii, hivyo marekebisho yake yanahitaji maoni ya wadau ili kufikia mwafaka.
Kwa upande wa wazee wa kimila, Katibu wa Mtandao wa Wazee wa Mila Tanzania, Chifu Girihuida Shulumbu anasema pamoja na kubadili sheria, jamii inapaswa kubadili mtazamo kuhusu thamani ya mtoto wa kike.
Anasema elimu ya mtoto wa kike ina manufaa makubwa kwa familia na taifa kuliko faida ya muda mfupi inayotokana na mahari.
Chifu wa Wafipa, Chifu Malema Sinyangwe anasema mila zinazolinda watoto zinapaswa kuendelezwa, huku zile zinazochochea ndoa na mimba za utotoni zikiondolewa.
Kwa upande wake, Askofu Ambele Mwaipopo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Ziwa Tanganyika anasema kuna mkanganyiko kati ya Sheria ya Ndoa na sheria nyingine zinazomtambua mtu mwenye umri chini ya miaka 18 kuwa mtoto.
Anasema wakati sheria nyingine zinalinda haki ya mtoto kupata elimu, afya na maendeleo, Sheria ya Ndoa bado inatoa mwanya wa mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 14 au 15 kwa masharti yaliyowekwa.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Sheikh wa Mkoa wa Rukwa, Rashid Akilimali anayehoji sababu ya kuwepo kwa kifungu kinachoruhusu mtoto kuolewa chini ya miaka 18 wakati sheria nyingine zinamtambua bado kuwa mtoto.
Serikali yaendelea na mchakato
Kwa upande wa Serikali, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Katimba anasema katika Mwaka wa Fedha 2026/2027 itaendelea na mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi kuhusu marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, ikiwamo Kifungu cha 13 kinachohusu umri wa mtoto wa kike kuolewa.
Anasema sheria hiyo ilitungwa mwaka 1971 baada ya mchakato wa ukusanyaji wa maoni kupitia White Paper na imefanyiwa marekebisho mara nne, mwaka 1974, 1980, 1996 na 2006.
Kwa mujibu wa Katimba, Serikali tayari imekusanya maoni katika baadhi ya mikoa, ikiwamo Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Lindi, Arusha, Dodoma na Mara lakini imebaini umuhimu wa kuwashirikisha wananchi wa mikoa iliyosalia.
“Baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, Serikali itawasilisha bungeni muswada ambao utakuwa umezingatia maoni ya wananchi,” anasema.
Anaongeza kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kulinda haki za watoto, ikiwamo kuboresha miundombinu ya elimu na kuhakikisha upatikanaji wa elimu bila malipo.
Kwa Monica, mjadala huu si wa sheria pekee, bali ni suala linalohusu maisha na mustakabali wa mtoto.
Anasema kama angekubali kuolewa akiwa na miaka 13, huenda asingepata nafasi ya kuendelea na masomo wala uwezo wa kufanya maamuzi kuhusu maisha yake.
“Ninaamini kila mtoto wa kike anapaswa kupewa nafasi ya kuchagua elimu badala ya kulazimishwa kuingia kwenye ndoa akiwa bado mtoto,” anasema.



