Silaha saba zasalimishwa

WAKAZI mkoani Tabora wameanza kuitikia wito wa Jeshi la Polisi wa kusalimisha silaha wanazomiliki kinyume cha taratibu.

Jumla ya silaha saba zimesalimishwa katika muda usiozidi wiki mbili tangu kuanza kwa kampeni hiyo.

Wakizungumza katika mikutano ya hadhara iliyoandaliwa na jeshi hilo katika wilaya za Nzega na Tabora Mjini kwa ajili ya hamasa na utoaji elimu kwa jamii, baadhi ya wananchi wamesema kampeni hiyo ni nzuri kwani itapunguza matukio ya uhalifu wa kutumia silaha ambayo yamekuwa yakiongezeka.

Mkazi wa Kata ya Busondo wilayani Nzega, Mohamed Makaranga, alisema kampeni hiyo itasaidia wananchi kuishi kwa amani na usalama.

Boniface Filipo (55) mkazi wa Kijiji cha Nkiniziwa, Kata ya Nkiniziwa wilayani Nzega, alisema ameamua kurejesha kwa hiari silaha aliyokuwa anamiliki aina ya gobore ili kutii agizo la serikali.

Alibainisha kuwa silaha hiyo ambayo aliachiwa na babu yake alikuwa anaitumia kulinda mifugo yake (ng’ombe 100) ila baada ya kuelimishwa umuhimu wa kumiliki silaha kihalali ameamua kuisalimisha hadharani.

Naye Mateo Sukamba (54) mkazi wa Kijiji cha Mbagwa, Kata ya Mbagwa ambaye ni mkulima alisema utaratibu wa Jeshi la Polisi kuitisha mikutano ya hadhara katika vijiji mbalimbali na kuwapa elimu umemgusa na kuamua kusalimisha silaha yake.

Alisema silaha hiyo aliuziwa na rafiki yake na alikuwa anaitumia kulinda mazao na mifugo yake (ng’ombe 60) ila ameamua kuisalimisha ili kutii agizo la serikali na kuongeza kuwa alikuwa hajui utaratibu wa kumiliki kihalali silaha.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Richard Abwao alisema utaratibu huo ulianza Septemba mosi mwaka huu na umezaa matunda kwani hadi sasa jumla ya silaha haramu saba aina ya gobore zimesalimishwa.

Alisema silaha zingine sita ambazo ni magobore manne na shot gun mbili zilizokuwa zikihusishwa na matukio ya kihalifu zimekamatwa kutokana na msako wa polisi na watuhumiwa wanne wametiwa mbaroni.

 

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button