Simba, Yanga kazi ipo kimataifa

TIMU za Yanga na Simba leo zinatarajiwa kushuka kwenye viwanja tofauti katika mechi za hatua ya awali za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Zote zitakuwa ugenini, Simba ikiwa Lilongwe, Malawi kumenyana na Nyasa Big Bullet kwenye Uwanja wa Taifa wa Bingu, huku Yanga ikimenyana na Zalan ya Sudan Kusini kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Timu za Sudan Kusini zinatumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa vile viwanja vya kwao havikidhi. Simba inacheza mechi hiyo ikiwa chini ya kocha mpya wa muda, Juma Mgunda aliyechukua mikoba ya Zoran Maki aliyefutwa kazi wiki iliyopita.

Kocha huyo mzawa aliyechukuliwa kutoka Coastal Union,aliizungumzia mechi hiyo na kusema, anaamini itakuwa ngumu kutokana na timu wanayokutana nayo, lakini amefurahi kuona wachezaji wa kikosi hicho wakiwa na morali.

Alisema japo amekabidhiwa timu hiyo juzi lakini anaamini kwa viwango na ubora wa wachezaji hao na kwa namna walivyompokea anaamini hatokuwa na wakati mgumu kwenye kuelekezana nini cha kufanya ili wapate ushindi.

“Nimewaona wapinzani wetu, sio timu ya kubeza, wana kikosi kizuri kinachocheza kitimu hivyo tunapaswa kufanya kazi ya ziada ili kuondoka na ushindi japo hata morali ya wachezaji wangu imenifurahisha na inachagiza upambanaji kuelekea mechi hiyo.

Upande wa Yanga, nahodha wa kikosi hicho, Bakari Mwamnyeto alisema wamekuwa na maandalizi mazuri kwa ajili ya mechi hiyo ambayo anaamini itakuwa ngumu kuliko iliyopita ya Ligi Kuu waliyoumana na Azam na kuisha kwa sare ya mabao 2-2. Alisema anafahamu benchi na wachezaji namna walivyojipanga kuwakabili wapinzani wao hao na kuhakikisha hawafanyi makosa ambayo pengine yanaweza kuwapa ugumu wa kutafuta matokeo na kwenda hatua inayofuata.

Timu nyingine itakayodondoka dimbani leo kwenye michuano hiyo ni KMKM ya Zanzibar itakayopepetana na Al Ahli Tripoli ya Libya kwenye Uwanja wa Amaani, Zanzibar kabla ya kurudiana Septemba 17, mwaka huu.

Aidha, kesho timu ya Geita Gold ya Geita itakuwa kibaruani kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiumana na Hilal Alsahil ya Sudan kwenye Uwanja wa Al Hilal uliopo Omdurman, Khartoum.

Nao Kipanga FC wawakilishi wengine kutoka visiwani Zanzibar watakuwa kibaruani dhidi ya Al Hilal Wau ya Sudan Kusini kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Wau watakuwa nyumbani katika mchezo huo kutokana na sababu zinazofanana na timu ya Zalan.​​​​​​​

Habari Zifananazo

Back to top button