Tanroads yatangaza zabuni njia nne Kibaha-Moro

SERIKALI kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imetangaza zabuni ya ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Kibaha – Mlandizi – Chalinze – Morogoro yenye urefu wa kilometa 205.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya alilieleza bunge jijini Dodoma Jumanne wakati akijibu swali la Mbunge wa Kibaha Mjini, Sylevester Koka (CCM).
Mbunge Koka alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuijenga kwa kiwango cha lami njia nane barabara ya Dar es Salaam hadi Morogoro.
“Barabara hiyo itajengwa kwa utaratibu wa Engineering, Procurement, Construct and Finance (EPC + F),” alisema.
Alisema gharama za ujenzi wake zitatolewa na serikali au na sekta binafsi (PPP) kwa utaratibu wa jenga, endesha, rudisha (BoT).
Katika utaratibu huo, sekta binafsi itajenga barabara hii kwa fedha zake na kuiendesha hadi pale itakaporejesha fedha zake kupitia tozo za magari.
Katika swali la nyongeza, Mbunge Koka alitaka kujua barabara ya Tamko- Mapinga imekuwa ikisuasua kwa muda mrefu na wananchi wa kata za Tangani na Pangani waliopisha ujenzi wa barabara hiyo lini watalipwa fidia.
Pia aliuliza: “Barabara ya zamani ya Dar es Salaam –Morogoro katika eneo la Picha ya Ndege-Mlandizi, imekuwa msaada mkubwa kunapotokea changamoto katika barabara kuu ya ajali magari hupita katika barabara hiyo, je, serikali ipo tayari kurekebisha barabara hiyo ili kuendelea kutumika wakati barabara kuu inapokuwa na changamoto?”
Kasekenya alijibu kwamba ni kweli barabara ya Tamko-Mapinga inasuasua na baadhi ya watu hawakulipwa fidia. Alisema serikali inalifahamu hilo na inalifanyia kazi ili kuhakikisha wananchi wanalipwa na ujenzi wake unakamilika kwa wakati.
Kuhusu barabara ya zamani ya Picha ya Ndege-Mlandizi kufanyiwa maboresho, alisema analichukua hilo kama wizara atazungumza na Tanroads ili kuangalia namna gani wanaweza kuboresha ili kuendelea kuwa msaada wa kukwamua msongamano unapotokea katika barabara kuu.