Tanzania yasisitiza usimamizi maeneo ya malisho

ULAANBAATAR: Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi endelevu wa maeneo ya malisho na rasilimali za udongo, huku ikieleza kuwa ukame, malisho kupita kiasi na mabadiliko ya tabianchi vinaendelea kuongeza tishio kwa maisha ya wananchi na usalama wa chakula.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, alitoa kauli hiyo jana, Agosti 26, 2026, wakati akishiriki kikao kuhusu afya ya udongo na matumizi sahihi ya mbolea kilichofanyika katika Ubalozi wa Uingereza jijini Ulaanbaatar, Mongolia.
Kikao hicho kilikuwa sehemu ya juhudi za kimataifa za kukabiliana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame.
Mhandisi Masauni alisema Tanzania inaendelea kuhimiza matumizi endelevu ya maeneo ya malisho, mipango shirikishi ya matumizi ya ardhi, urejeshaji wa maeneo yaliyoharibiwa, uboreshaji wa miundombinu ya maji, mifumo ya tahadhari ya mapema ya ukame na kuimarisha uzalishaji wa mifugo.
“Tunatoa elimu kuhusu tabianchi, maendeleo na uwekezaji, huku tukihamasisha ubia kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuharakisha urejeshaji wa maeneo ya malisho na kuhakikisha kila mmoja anawajibika katika kulinda udongo,” alisema.
Alisema maeneo ya malisho ni muhimu kwa uzalishaji wa mifugo nchini, usalama wa chakula, uhifadhi wa bioanuai, vyanzo vya maji na maisha ya wananchi wa vijijini.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Tanzania yenye wakazi wanaokadiriwa kufikia milioni 61.7 inaendelea kukabiliwa na ongezeko la shinikizo kwenye ardhi, maji na rasilimali nyingine za asili.
Alisema takwimu za Utafiti wa Sampuli ya Kilimo wa Mwaka 2022/23 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), zinaonesha kuwa Tanzania ilikuwa na takribani kaya milioni 8.97 za kilimo, ambapo asilimia 60.6 zilijihusisha na ufugaji.
Mhandisi Masauni alisema takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuhakikisha maeneo ya malisho yanasimamiwa vizuri kwa manufaa ya jamii na uchumi wa taifa.
Hata hivyo, alisema maeneo hayo yanaendelea kukabiliwa na changamoto zinazotokana na ukame, uharibifu wa ardhi, malisho kupita kiasi, mabadiliko ya matumizi ya ardhi, upungufu wa maji, moto wa misitu na mabadiliko ya tabianchi.
Alisema Tanzania imechukua hatua kukabiliana na changamoto hizo kupitia Programu ya Taifa ya Kukabiliana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame ya mwaka 2025–2030, inayolenga kuimarisha maandalizi dhidi ya ukame, mifumo ya tahadhari ya mapema na usimamizi endelevu wa ardhi.
Mhandisi Masauni alisema hatua hizo pia zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan nguzo ya tatu inayolenga uhifadhi wa mazingira na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Alisema nguzo hiyo inaunganisha urejeshaji wa maeneo ya malisho na mageuzi katika sekta ya mifugo, usalama wa chakula na kuimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mhandisi Masauni yuko nchini Mongolia kushiriki Mkutano wa 17 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa (UNCCD COP17), ulioanza Agosti 24, 2026.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mwakilishi Maalum wa Uingereza nchini Mongolia, Ruth Davis; Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Beth Bechdol; Kamishna wa Umoja wa Afrika anayesimamia Kilimo, Maendeleo ya Vijijini, Uchumi wa Buluu na Mazingira Endelevu, Moses Vilakati, pamoja na wawakilishi kutoka nchi mbalimbali.



