Tanzania yataka uwekezaji ardhi iliyoharibika

TANZANIA imeitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza uwekezaji, teknolojia na rasilimali fedha kwa ajili ya kurejesha ardhi iliyoharibika na kukabiliana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame, huku ikisisitiza umuhimu wa kulinda maeneo ya malisho, misitu na vyanzo vya maji.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, wakati Tanzania ikishiriki Mkutano wa 17 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa (UNCCD COP17), uliofunguliwa rasmi Jumapili jijini Ulaanbaatar na Rais wa Mongolia, Khurelsukh Ukhnaa.

Mhandisi Masauni amesema mkutano huo wenye kaulimbiu “Rejesha Ardhi, Rejesha Matumaini” unaweka mkazo katika kuongeza uwekezaji wa kurejesha ardhi, kujenga uwezo wa kukabiliana na ukame na kuenea kwa hali ya jangwa, pamoja na kusimamia maeneo ya malisho kwa njia endelevu.

Amesema kutangazwa kwa mwaka 2026 kuwa Mwaka wa Kimataifa wa Maeneo ya Malisho na Wafugaji kumeongeza uzito wa ajenda ya Tanzania kuhusu uhifadhi wa maeneo ya malisho na ustawi wa jamii za wafugaji katika mkutano huo.

“Kwa Tanzania, uharibifu wa ardhi unasababishwa na mambo mbalimbali, yakiwemo ukataji na uharibifu wa misitu, upanuzi wa shughuli za kilimo, uchomaji moto holela, mmomonyoko wa udongo, matumizi yasiyo endelevu ya ardhi na upanuzi wa makazi,” amesema.

Mhandisi Masauni amesema ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo unatoa fursa ya kupata uzoefu, teknolojia, ushirikiano na rasilimali fedha zitakazosaidia kuimarisha usimamizi endelevu wa maeneo ya malisho, kurejesha ardhi iliyoharibika, kuhifadhi misitu na vyanzo vya maji, kulinda bayoanuai na kuongeza uwezo wa wakulima na wafugaji kukabiliana na changamoto za mazingira.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Kitaifa wa Mkataba huo Tanzania, Thimoth Mande, amesema ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika kuiwezesha Tanzania kukabiliana na uharibifu wa ardhi, upotevu wa bayoanuai na mabadiliko ya tabianchi kwa mtazamo jumuishi badala ya kushughulikia changamoto hizo kwa kutenganisha.

Amesema ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo hauishii katika kuhudhuria pekee, bali pia unatoa fursa ya kuonesha hatua ambazo tayari zinatekelezwa nchini katika kukabiliana na uharibifu wa ardhi, huku ikitafuta uwekezaji na teknolojia zaidi.

Kwa mujibu wa Bw Mande, Tanzania inaweza kutumia matokeo ya mkutano huo kuhamasisha rasilimali zaidi kutoka taasisi na mifuko ya fedha za mazingira, ikiwemo Global Environment Facility (GEF), International Fund for Agricultural Development (IFAD), United Nations Development Programme (UNDP), Food and Agriculture Organisation (FAO) na United Nations Environment Programme (UNEP).

Amesema rasilimali hizo, pamoja na uwekezaji kutoka sekta binafsi na mifumo bunifu ya fedha, zinaweza kusaidia kupanua miradi ya kurejesha ardhi kutoka maeneo mahususi hadi katika maeneo makubwa zaidi.

Naye, Meneja wa Kanda ya Mashariki na Kusini wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Bi Aminata Kirama, amesema baraza hilo linaendelea kufanya tafiti na kutathmini maeneo yanayokabiliwa na changamoto za kimazingira ili kutoa msingi wa kuchukua hatua sahihi za uhifadhi na urejeshaji wa ardhi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button