‘Tunaendelea kuwakabili panya road msishituke milio ya risasi’

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro

KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amewataka wakazi wa mkoa huo kutokuwa na hofu wanaposikia milio ya bunduki usiku kwani oparesheni ya kukamata vikundi vya uhalifu maarufu kama panya road, inaendelea.

Alisema hayo baada ya wakazi wa maeneo ya Chamazi na Mgeninani Kijichi wilayani Temeke mkoani humo kueleza kuwa Jumatatu usiku ya wiki hii walisikia milio ya bunduki na kusababisha hofu.

Akizungumza na HabariLEO, Muliro alisema kazi ya Jeshi la Polisi ni kuhakikisha wananchi wanakuwa salama, hivyo wahalifu wanapaswa kukaa chonjo kwani matumizi ya silaha yatatumika endapo watashindwa kujisalimisha.

Advertisement

Alisema polisi wanaendelea na oparesheni ya kuwakamata panya road katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo na kwamba itatoa taarifa walipofikia katika oparesheni hiyo.

“Tunatembea na silaha, si mishale kwa hiyo watu wanaposikia milio ya bunduki wasishituke kwa sababu bado tupo kazini. Kama kuna taarifa za vifo pia tutawaita na kuwajulisha,” alisema.

Mmoja wa dereva bodaboda maeneo ya Saku Chamazi, Waziri Juma alisema juzi usiku polisi walifanikiwa kusambaratisha kikundi cha watu ambao walikuwa wamekaa kwenye pagale.

Alisema vijana hao wamekuwa wakivuta bangi na kusubiri kufanya matukio wakati wa usiku, hivyo katika doria inayoendelea polisi iliwalazimu kutumia bunduki kupiga juu ili wawakamate.

“Yaani kitendo cha polisi kuwakamata na kuwaua panya road ninakifurahia sana kwa sababu vijana hawa kwanza ni wadogo lakini wamekuwa wakitusumbua kwa matukio yao ya uhalifu, hatuna amani hata kidogo,” alisema.

Alieleza kuwa: “Juzi waliwaua panya road kama wanane hivi maeneo hayahaya ya Chamazi, lakini pia kuna kijana mmoja alikamatwa nyumbani kwao usiku na kuchukuliwa na maofisa usalama akidaiwa kushirikiana na panya road mpaka sasa hajarudi na wazazi wake wamemtafuta vituo vyote vya polisi na hospitali hawajampata.”

Mkazi wa Mgeninani Kijichi, Mussa Seif alisema kuwa Jumatatu polisi mbalimbali walikuwa na oparesheni katika maeneo yao hivyo risasi zilirindima usiku katika majibizano na majambazi.

Alisema hali hiyo inatia hofu kwa sababu hawajazoea lakini wanaamini Jeshi la Polisi litawakamata wahusika ili kuendelea na utulivu uliokuwapo awali.

Mfanyabiashara wa mitumba, Leonard Charles alisema wakati akirejea nyumbani kwake Kilungule usiku baada ya shughuli zake, alikutana na kundi la wahalifu waliomsimamisha na kumtaka kuwapa kila kitu alichonacho.

Juzi, Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla alisema watu 135 wamekamatwa ndani ya siku nne katika oparesheni iliyoanza Septemba 15 ikilenga kutokomeza vikundi vya uhalifu vilivyoibuka na kuvamia mitaa mbalimbali, kupora mali, kujeruhi na hata kuua.