‘Tutaendelea kuboresha sheria utekelezaji Dira 2050’

DODOMA; Serikali imesema itaendelea kufanya maboresho ya sheria, ili kuhakikisha kuwa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 iliyopitishwa na Bunge inatekekelezwa ipasavyo.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Septemba 2, 2026 na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, alipokuwa akiwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 wa Mwaka 2026.
“kwa mara nyingine naomba, kwa niaba ya serikali, niliahidi Bunge lako tukufu kuwa serikali itaendelea kufanya maboresho ya sheria ili kuhakikisha kuwa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 iliyopitishwa na Bunge lako tukufu inatekekelezwa ipasavyo,” amesema Johari.
Amesema muswada huo unapendekeza marekebisho katika Sheria Kuu Saba, ambazo ni Sheria ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Sura ya 116, Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287; Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288.
Nyingine ni Sheria ya Baraza la Usalama la Taifa, Sura ya 61, Sheria ya Mamlaka ya Nchi Katika Umiliki wa Mali na Rasilimali Asilia, Sura ya 449; Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini, Sura ya 138; na Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, Sura ya 283.



