Asilimia 91 ya watoto 68 waliofanyiwa uchunguzi katika kambi maalumu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) wamekutwa na matatizo ya moyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dk Alphonce Chandika, amewaambia waandishi wa habari leo, Jumatano jijini Dodoma kuwa watoto 18 wamefanyiwa upasuaji kwa njia ya matundu kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa moyo kutoka Marekani.
“Matibabu haya yamefanyika bure katika kambi hii maalumu,” amesema Dk Chandika.
BMH inaendesha kambi hiyo ya wiki moja kwa ushirikiano na Shirika lisilo la Kiserikali la One New Heart Tanzania & USA.
Mtaalam huyo ametaja baadhi ya matatizo waliyokutwa nayo kwenye moyo watoto hao ni pamoja na matundu kwenye moyo na matatizo kwenye mishipa ya moyo na matatizo kwenye njia ya moyo.
Mama Specioza Anthony, mmoja wa wazazi wanufaika wa kambi hiyo, ameishukuru BMH kwa zoezi hilo.
“Nashukuru Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa huduma hii maana ningetoa wapi mimi milioni saba ya upasuaji kwa mtoto?,” alihoji Mama Specioza, mkazi wa Chato, mkoani Geita.
Naye Nickson Rwekaza, mzazi mwingine mnufaika, ametoa wito kuwa hospitali nyingine kuiga mfano wa BMH kwa kwa kuandaa kambi maalum za matibabu.
“Nawapongeza Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kambi hii maalumu na hospitali nyingine waige mfano huu,” amesema mkazi huyo wa Kagera.