UCSAF kufunga intaneti ya bure vituo vya afya

GEITA; SERIKALI kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeanza kutekeleza mradi wa huduma ya intaneti ya bure kwenye maeneo ya wazi ikiwemo masoko na vituo vya afya mkoani Geita.
Mkuu wa UCSAF Kanda ya Ziwa, Fredy Kandonga alieleza hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya mawasiliano Mkoa wa Geita mbele ya Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).-
Amesema maeneo hayo yanatarajiwa kufungiwa mtandao wa intaneti na kuwezesha watumiaji wa maeneo hayo kupata huduma ya intaneti bure kwa makubaliano na mtoa huduma.
“Tunatoa ruzuku kwa mwaka mmoja baada ya hapo tunategemea mamlaka inayohusika iendelee kutoa huduma,” amesema Kandonga.
Kandonga amesema kwa mwaka wa fedha 2025/26 maeneo mawili yaliingizwa kwenye mradi huu ambayo ni soko la Ushirombo wilayani Bukombe na Hospitali ya Wilaya ya Geita, Nzera.
Ameongeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2026/27 UCSAF inaendelea na mradi mkoani Geita ambapo maeneo yaliyolengwa ni Hospitali ya Wilaya ya Chato, na Kituo cha Afya cha Katoro.
“Maeneo ya Soko la Ushirombo pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Geita tayari ipo kwenye hatua ya ununuzi, lakini kwa Hospitali ya Wilaya ya Chato na Kituo cha Afya Katoro ipo hatua za awali,” amesema.
Amesema ili kuimarisha huduma ya mawasiliano katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa minara 758 katika kata 688.
Kandonga amesema katika kuboresha huduma ya intaneti ndani ya miaka minne serikali imefanikiwa kuongeza nguvu ya minara 304 kutoka teknolojia ya 2G hadi 3G au 4G.
“Kwa upande wa Mkoa wa Geita, Serikali kupitia UCSAF ilitenga ruzuku ya Sh bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa minara 19 katika kata 17 kupitia mradi wa Tanzania ya Kidigitali.
“Hadi kufikia Desemba 31, 2025 minara yote kwenye kata 17 tayari ilikuwa imekamilika na inatoa huduma za mawasiliano”, amesisitiza Kandonga.
Mwenyekiti wa Kikao cha RCC, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Pasikasi Muragili ameiomba UCSAF kuendelea kufanya utafiti ili kuimarisha mawasiliano kwenye maeneo yenye changamoto.



