Uwekezaji mradi wa HEET washika kasi SUA

MOROGORO: CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kinaendelea kufanya ukarabati mkubwa wa miundombinu na ujenzi wa majengo mapya kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Ujenzi huo unafanyika katika kampasi tatu za chuo ili kupanua uwezo wa kudahili wanafunzi na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
Mtaalamu na Msimamizi wa Ujenzi wa Mradi wa HEET kutoka SUA, Mhandisi Japhet Maduhu,amesema hayo wakati wa ziara ya kutembelea ili kuona maendeleo ya ujenzi na ukarabati wa majengo katika Kampasi ya Mizengo Pinda (Katavi), Kampasi ya Solomon Mahlangu (Mazimbu) na Kampasi ya Edward Moringe zilizopo Morogoro.

Mhandisi Maduhu ameeleza kuwa lengo la mradi huo ni kufanikisha dhima ya kufufua na kupanua uwezo wa vyuo vikuu katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
Amesema mradi unahusisha ujenzi wa majengo mapya tisa, yakiwemo majengo matatu ya maabara, hosteli mbili, na majengo manne kwa ajili ya shughuli za kitaaluma.
Mhandisi Maduhu amesema licha ya ujenzi wa majengo hayo mapya majengo mengine ya zamani 18 yanakarabatiwa ili yaendane na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia, kwa kuweka mifumo mipya ya TEHAMA na umeme, badala ya miundombinu ya zamani iliyokuwepo.

“Tangu tumeanza utekelezaji wa mradi huu kwa ujumla kwake umefikia zaidi ya asilimia nane na Wakandarasi wote wako kazini na wanaendelea na shughuli za ujenzi. Kwa kasi kubwa” amesema Mhandisi Maduhu.
Mhandisi Maduhu amesema kwa upande wa Chuo Kikuu hicho kimepewa na Serikali kuu kiasi cha Sh bilioni 73.6, ambapo takribani Sh bilioni 58 zimeelekezwa kwenye shughuli za ujenzi kwa kampasi zote tatu.
Amesema kuwa ukarabati wa majengo unatekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja, ambao ulianza Desemba mwaka jana (2024) na kutarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu (2025) wakati ujenzi wa majengo mapya,unatarajiwa kuchukua miezi 18, na kukamilishwa ifikapo Juni 2026.

Naye Msimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa Kampasi ya Solomon Mahlangu, Mhandisi Enock Kamagu, amesema ujenzi unaendelea vizuri licha ya changamoto ya mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Morogoro.
Mhandisi Enock amesema kuwa ,awali mkandarasi alikumbwa na changamoto ya ucheleweshaji wa vifaa vya ujenzi, lakini kwa sasa hali imeimarika na wana imani kuwa kazi itakamilika kwa wakati.
Naye Mhandisi wa ujenzi wa Kampuni ya JIC – China Jiangx ,Peter Kulwa amesema wamepewa kazi ya ujenzi wa majengo mapya katika Kampasi ya Solomon Mahlangu na hadi sasa wamefikisha miezi mitano ya utekelezaji wa ujenzi ambapo utakamilishwa kwa muda uliopangwa ndani ya mkataba.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko SUA, Suzana Magobeko, amesema kukamilika kwa mradi huo wa ujenzi kutachochea ongezeko la udahili wa wanafunzi katika kampasi zote tatu za chuo hicho, pamoja na kupanua fursa zaidi za kuwafikia wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Suzana amesema kuwa uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia, kujifunzia na kufanya utafiti utaongeza ubora wa mafunzo, na kuwasaidia Wahadhiri na watafiti kufikia malengo yao.



