Vituo vya ubunifu kuwa Injini za biashara na ajira

MOROGORO: Serikali imeeleza kuwa itaendelea kuweka mazingira wezeshi katika vituo vya ubunifu na kongani za biashara ili kuhakikisha havibaki kuwa maeneo ya mafunzo pekee, bali vinakuwa chachu ya kuzalisha biashara zinazokua, kutengeneza ajira, kuongeza mauzo ya nje na kuchangia ukuaji wa uchumi na pato la taifa.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo amesema hayo leo Julai 21, wakati wa ufunguzi wa kongamano la kitaifa kuhusu mchango wa vituo vya ubunifu na kongani za biashara katika kukuza biashara ndogo na kati (SMES)Tanzania ambalo limeandaliwa na Taasisi ya Uongozi.

Londo amesema miongoni mwa mambo yaliyofanyika ni maboresho ya kanuni za kikodi  zipatazo 374 zilitokana na Mapendekezo ya Tume ya Rais ya kikodi  kwa lengo la kuvutia wawekezaji  kuwekeza  katika sekta mbalimbali.

Naibu Waziri ametaja eneo lingine ni kuendelea kuboresha mazingira ya biashara kupitia mageuzi ya sera, sheria na kanuni ili kupunguza urasimu na gharama za kufanya biashara.

Amesema Serikali  itaendelea kuimarisha upatikanaji wa fedha kwa biashara ndogo kupitia ushirikiano na taasisi za fedha, mifuko ya maendeleo, benki za biashara na mifumo ya dhamana za mikopo kwa biashara ndogo na za kati.

Pia itaendelea kuimarisha na kuanzisha vituo vya ubunifu na kongani za biashara zinazojikita katika sekta zenye fursa kubwa kama vile uchakataji wa mazao ya kilimo, madini, ngozi, dawa, teknolojia za kidijitali, uchumi wa buluu, nishati safi na viwanda vya ubunifu.

Naibu Waziri ametaja eneo lingine ni kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya viwanda, TEHAMA, nishati na usafirishaji ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ushindani wa biashara za ndani.

“Tunaendelea kuimarisha taasisi kama SIDO, COSTECH, TIRDO, VETA, NEEC na taasisi nyingine ziweze kutoa huduma bora zaidi kwa wajasiriamali na biashara ndogo”  amesema Londo.

Naye  Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi , Kadar Singo amesema jukumu la taasisi hiyo ni kutoa mafunzo kwa viongozi, kufanya tafiti tumizi, kuandaa mijadala ya kisera, pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa taasisi za umma na binafsi.

Singo amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, ilifanya utafiti kuhusu mchango wa vituo vya Ubunifu na Kongani za Biashara katika kukuza biashara ndogo na za kati nchini Tanzania.

Singo amesema utafiti huo ulilenga kuelewa mchango wa vituo vya ubunifu na kongani za biashara katika kukuza ujasiriamali, kuongeza ubunifu, kurahisisha upatikanaji wa teknolojia, mitaji, masoko na huduma za ushauri kwa biashara ndogo na za kati.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendajiwa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) ,Mwajuma Hamza amesema kuwa asilimia 78 ya biashara hapa nchini zinaendeshwa nje ya mfumo rasmi.

Hivyo  kupitia kongamano hilo ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kuweka mfumo mmoja utakaotumiwa na taasisi mbalimbali zinazotoza tozo  na leseni unaosomana ili kuondoa usumbufu wa kibashara.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button