Wadau sheria wazungumzia faragha kwa wafungwa

SERIKALI imeshauriwa kujifunza katika nchi nyingine zinavyofanya kutoa haki ya faragha kwa wafungwa na wenza wao.

Aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk Rugemeleza Nshalla, alisema suala la utu linazungumzwa katika Ibara ya 12 na 13 ya Katiba ya Tanzania.

Alisema Watanzania hawana budi kuangalia namna sheria zao zinavyoheshimu utu wa watu kwa mujibu wa katiba

Advertisement

“Kuna haja ya kuangalia wenzetu katika nchi nyingine wanafanyaje ili tusogee mbele, kwa hiyo kuna haja ya kuboresha mazingira ya magereza ili watu wetu wasiwekwe kule kama wanyama tu,” alisema Dk Nshalla

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, alisema ni haki kwa wafungwa kuwa na faragha na wenza wao. Hata hivyo alisema jambo hilo linapaswa liende taratibu kwa kuwa si kitu rahisi.

Henga alisema haki za namna hiyo ni aina ya haki ambazo si kipaumbele kwa kuwa ni haki ya pili.

“Inabidi kutimiza kwanza haki za msingi kama utu wakiwa magerezani, kwa mfano mazingira safi na yenye mahitaji muhimu, magereza mpaka leo hakuna mahitaji maalumu kama malazi, wanalala kwa kubanana na hakuna mavazi ya kutosha,”alisema Henga

Wakili wa kujitegemea, Reuben Simwanza, alisema kwa mujibu wa haki za binadamu, suala la faragha ni haki ya wafungwa na mahabusu.

Alisema wafungwa na mahabusu kuwekwa gerezani au mahabusu iwe ni katika kudhibiti uhuru wao wa matembezi na mambo mengine lakini faragha ni muhimu kwao kama binadamu.

Simwanza alisema kwa kuwa katika nchi za Afrika kuna vitu watu wanahitaji kuviona vikifanyika likiwamo suala la faragha, bado ni vigumu kufanyika.

Alisema ikiwa mpaka sasa mtu akitaka kuongea na mfungwa au mahabusu bado anatumia dirisha,  kuzungumzia suala la kuwa na vyumba kwa ajili ya faragha  litasubiri kwa sababu halipewi kipaumbele.

Hivi karibuni, serikali ilisema haki ya faragha kwa wafungwa na wenza wao itaanza kutolewa mifumo ya kisheria na miundombinu ya magereza itakapokidhi mahitaji hayo.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alisema bungeni Dodoma kuwa serikali inaendelea kutoa haki kwa wafungwa magerezani kwa mujibu wa sheria.

Masauni alisema haki ya msingi ya wafungwa ni chakula na malazi na si haki ya faragha kwani kuna mambo ya msingi ya kuzingatia.

Alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Bahati Ndingo aliyetaka kufahamu serikali itaweka lini mfumo utakaoruhusu wafungwa kupata haki ya faragha na wenza wao.