Wafungwa Mbeya waomba kurasimishiwa ujuzi wao

MBEYA: Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kupitia Chuo cha VETA Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza mkoani humo, imeanza mchakato wa kutambua, kutathmini na kurasimisha ujuzi wa ufundi stadi kwa wafungwa 100 walioupata wakati wakitumikia vifungo vyao.

Mchakato huo ulianza Agosti 27, 2026, katika Chuo cha Ufundi cha Jeshi la Magereza Ruanda jijini Mbeya na unatarajiwa kukamilika Septemba 15, 2026, huku washiriki wakifanyiwa tathmini kulingana na stadi walizonazo.

Akizungumza kuhusu mchakato huo, Meneja wa Kanda ya Kusini Magharibi wa VETA, Shomari Chololo, amesema waombaji hao wamegawanyika katika stadi mbalimbali, zikiwemo ufundi umeme wanane, ufundi bomba 10, useremala 15, uashi 41, uungaji na uundaji vyuma 12, ushonaji 11 pamoja na huduma za ndani, usafi na utengenezaji wa sabuni watatu.

Amesema wafungwa watakaokidhi vigezo baada ya kufanyiwa tathmini watapatiwa vyeti vinavyothibitisha ujuzi wao, hatua itakayowawezesha kutumia ujuzi huo kwa tija baada ya kumaliza vifungo, ikiwemo kujiajiri, kuajiriwa au kuanzisha shughuli za uzalishaji.

Mchakato huo ni sehemu ya programu ya Utambuzi na Urasimishaji Ujuzi uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo (RPL), inayotekelezwa na VETA kwa lengo la kutambua na kuthibitisha ujuzi unaopatikana kupitia mafunzo na uzoefu wa vitendo.

Kupitia RPL, wahusika hufanyiwa tathmini ya uwezo wao katika stadi husika, kubainishwa maeneo yenye upungufu na kupewa mafunzo ya muda mfupi ili kuziba mapungufu hayo kabla ya kutunukiwa vyeti vya urasimishaji ujuzi.

Hatua hiyo inatarajiwa kuwawezesha wafungwa hao kuwa na uthibitisho rasmi wa ujuzi wao wa kiufundi na kuongeza fursa za kiuchumi na ajira baada ya kumaliza kutumikia vifungo vyao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button