Wakulima 37 wafaidika mpango wa EFTA

ARUSHA; Wakulima 37 kutoka maeneo mbalimbali nchini wamepokea takribani Sh milioni 100 kama rejesho la asilimia 50 ya riba waliyolipa kupitia ufadhili wa EFTA, baada ya kurejesha kwa wakati.
Hafla ya kukabidhi hundi za mfano ilifanyika katika banda la EFTA kwenye Maonesho ya Nanenane jijini Arusha.

Wanufaika wa mpango huo walisema ufadhili wa EFTA umewawezesha kupata matrekta na mashine za uchakataji wa mazao, hatua iliyoongeza uzalishaji, kupunguza gharama za kilimo na kufungua fursa za ajira zaidi ya 300 katika maeneo mbalimbali nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa EFTA, Nicomed Bohay, alisema mpango huo unalenga kujenga utamaduni wa nidhamu ya kifedha kwa wakulima.



