Wamiminika kupata matibabu ya kibingwa Haspitali Kanda ya Mtwara

WAGONJWA 300 wamepata matibabu ya kibingwa yaliyoanza kutolewa katika hospitali ya Kanda ya Kusini mkoani Mtwara.

Hospitali hiyo ambayo ujenzi wake ulikamilika  Oktoba mwaka jana na kuanza kutoa huduma mbalimbali za matibabu imepokea madaktari bingwa wa mifupa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wenye matatizo ya mifupa  Kanda ya kusini.

Kaimu Mkurungenzi wa Hospitali hiyo Dkt Geoffrey Ngomo amesema madaktari hao walianza kutoa huduma za kibingwa jumatatu ya wiki hii ambapo walipokea wagonjwa 185, na jana jumanne walipokea wengine 115 wenye tatizo ya mifupa na magonjwa matatizo mengine ambayo yanahitaji upasuaji.

Ngomo  amesema, madaktari hao wameungana na madaktari bingwa hospitalini hapo kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa za mifupa watafanya upasuaji mpaka ijumaa na kwamba huduma hiyo itakuwa ni endelevu.

Wakiongea kwa nyakati tofauti wagonjwa waliofika hospitalini wameeleza kufurahishwa na hatua ya kuleta huduma za tiba kwa wagonjwa wenye matatizo ya mifupa na ambao wanahitaji upasuaji.

“Mimi kwanza nashukuru sana kwa serikali yetu kutuletea huduma za kibingwa hapa hapa Mtwara, tumepata faraja kubwa kwa sababu tulikuwa tunatumia gharama kubwa  kufuatilia matibabu Dar es Salaam,” amesema Fakina Mohammed ndugu wa mgonjwa ambaye amekuwa wa kwanza kufanyiwa upasuaji katika hospitali hiyo.

Wananchi pamoja na wagonjwa waliofika hospitalini hapo kupata huduma wameomba serikali kufanya huduma hiyo ya matibabu ya kibingwa kuwa endelevu ili kuwasaidia wananchi wengi ambao wanatumia gharama kubwa kwenda Muhimbili na MOI.

Habari Zifananazo

Back to top button