Wanafunzi kunufaika ufadhili Rotary

DAR ES SALAAM: Wanafunzi 150 wenye uhitaji wanatarajiwa kunufaika na ufadhili wa masomo kupitia mbio za mbuzi za mwaka 2026 zinazoandaliwa na Klabu ya Rotary ya Dar es Salaam Oyster Bay, huku klabu hiyo ikilenga kukusanya Sh milioni 250 kwa ajili ya kuwawezesha kuendelea na elimu ya juu.
Tukio hilo la kila mwaka la kuchangisha fedha kwa ajili ya shughuli za kijamii linatarajiwa kufanyika Septemba 19, 2026 katika Viwanja vya Posta Kijitonyama, Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rais wa Klabu ya Rotary Dar es Salaam Oyster Bay, Philippe Demoulin, amesema lengo la mwaka huu ni kuongeza kiasi cha fedha kitakachopatikana ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.
Amesema mwaka jana mbio hizo zilikusanya Sh milioni 158 baada ya gharama za uendeshaji, fedha zilizotumika kugharamia ada na mahitaji mengine ya kielimu kwa wanafunzi walionufaika.
“Tunatarajia kuongeza kiasi hicho hadi Sh milioni 250 mwaka huu ili kuwawezesha wanafunzi wengi zaidi kupata fursa ya elimu ya juu,” amesema.
Demoulin amesema mpango huo wa ufadhili umekuwa ukikua kwa miaka ya hivi karibuni, ambapo wanafunzi 26 walinufaika mwaka 2023, 43 mwaka 2024 na 92 mwaka 2025.
Amesema hadi sasa klabu hiyo imewahi kusaidia zaidi ya wanafunzi 400 kupitia mpango huo wa ufadhili wa masomo.
Kwa mujibu wa Demoulin, wanafunzi wanaonufaika huchaguliwa kwa kuzingatia ufaulu wao kitaaluma pamoja na hali ya kiuchumi ya familia zao, kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wenye vipaji hawaachwi nyuma kutokana na changamoto za kifedha.
“Tunayaandaa mashindano haya kama watu wa kujitolea, si kwa ajili ya kujinufaisha, bali kusaidia jamii na kuwawezesha vijana kupitia elimu,” amesema.
Klabu hiyo imewahimiza kampuni, taasisi na wananchi kushiriki kuchangia ili kufikia lengo la Sh milioni 250 na kuwawezesha wanafunzi 150 kupata ufadhili wa masomo ya elimu ya juu.



