Wananchi waomba ujenzi nyumba ya mganga mfawidhi Mnyahi

MTWARA: WAKAZI wa Kata ya Milango Minne iliyopo Halmashauri ya Mji Nanyamba wameiomba serikali kuwasaidia nyumba ya mganga mfawidhi wa Zahanati ya Mnyahi ili wakazi hao wapate huduma hiyo kwa urahisi.
Wamezungumza hayo September 8, katika mwendelezo wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, Abdallah Chikota jimboni humo, kiwa na lengo la kuwashukuru wananchi hao kwa kuendelea kukichagua Chama cha Mapinduzi (CCM).
Katika ziara hiyo, Chikota amekuwa akisikiliza changamoto mbalimbali zinazowakumba wananchi wa kata hiyo ikiwemo wa kijiji hicho cha Mnyahi, Mkumbwanana, Mnyawi sokoni, Milangominne na Umoja ili zifanyiwe kazi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi ikiwemo hilo la afya na mengine.

Miongoni mwa wananchi hao akiwemo Abdulazizi Mjupa mkazi wa kijiji cha mnyahi kwenye kata hiyo amesema kwa sasa mganga aliyopo anaishi nje ya maeneo ya kituo chake cha kazi.
“Kutokana na changamoto hii naeendelea kuiomba serikali kufanya kila linalowezekana kututatulia changamoto hii ili tupate huduma katika mazingira rahisi”amesema Mjupa.

Pia Mwanaidi Mohamedi mkazi wa kijiji hicho amesema kitendo cha mganga huyo kuisha nje ya zahanati hiyo ni changamoto kwao hasa kwa akina mama wajawazito wanapotaka kujifungua.
“Uchungu haupigi hodi Kwa sisi akina mama tunapotaka kujifungua kwahiyo tukifika pale zahanati inabidi tumpigie simu mganga na ukimpigia anakuja ila kama unavyojua mambo ya uchungu hauna kusubiri ukija umekuja”amesema Mwanaidi
Akitolea majibu kuhusu changamoto hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Hamza Hatibu amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027 halmashauri imetenga bajeti ya Sh milioni 17 na nguvu za wananchi ni zaidi ya takribani Sh milioni 10 hivyo kufanya jumla ya zaidi ya takribani Sh milioni 50 mpaka kukamilika kwake.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Hassan Mauji amewaomba wananchi hao kuwa na subra wakati serikali inapoendelea na utaratibu wa kukamilisha ujenzi wa mradi huo pamoja na miradi mingine ya maendeleo kwani maendeleo ni mchakato.



