Wanawake GGML waendesha semina kwa wanafunzi

KATIKA jitihada za kuhakikisha jamii inanufaika kutokana na shughuli za uchimbaji dhahabu nchini, wafanyakazi wanawake wa Kampuni ya Geita Gold Mine Limited (GGML) wameendesha semina ya siku mbili kwa ajili ya kutoa malezi ya kitaaluma kwa wanafunzi wa kike mkoani Geita.

Semina hiyo ilifanyika Jumamosi Mjini Geita katika Shule ya Sekondari ya bweni ya wasichana ya Nyankumbu iliyojengwa na GGML.

Akizungumza kwa niaba ya menejimenti ya GGML, Meneja Mwandamizi Mawasiliano na Mahusiano, Manace Ndoroma aalisema Umoja wa Watumishi Wanawake wanaofanya kazi mgodini unaojulikana kwa jina la GGM ladies wameamua kutoa mafunzo hayo kuonesha umuhimu wa nafasi ya mwanamke katika jamii.

Katika mafunzo hayo wametoa hamasa kwa mwanamke anayefanya shughuli zinazotokana na uchimbaji madini au biashara inayotokana na mnyororo wa thamani katika sekta ya uchimbaji kuwa imara katika nafasi zote .

Amesema GGML kupitia umoja huo imekuwa ikitoa misaada ya hali na mali ikiwemo fedha na vifaa mbalimbali kwa makundi maalumu ndani ya jamii ili kuhakikisha jamii inayozungukwa na shughuli za uchimbaji wa dhahabu inafaidika kutokana na uwepo wa kampuni hiyo.

“Tumekuwa mstari wa mbele kushirikiana na serikali kuhamasisha masuala ya usawa wa kijinsia. Mtakumbuka Agosti 26 mwaka huu ilikuwa siku ya usawa wa wanawake duniani. GGML tulitoa elimu kubwa kwenye mitandao yetu ya kijamii na vyombo vya habari juu ya nafasi muhimu ya mwanamke katika jamii”.

Alisema kumekuwepo changamoto ya wasichana wengi hususani katika mwaka wao wa mwisho wa masomo au baada ya kumaliza elimu ya sekondari kushindwa kufahamu hatima ya masomo wanayoyasomea na uhalisia wa watakachokutana nacho katika elimu ya juu au baadaye kwenye soko la ajira.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Profesa Godius Kahyarara amewataka wadau mbalimbali nchini kuchangia maendeleo ya elimu hususani kwa mtoto wa kike badala ya kuiachia serikali jukumu hilo peke yake.

Akihamasisha wanafunzi kufikia ndoto zao katika Shule ya Wasichana Nyankumbu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita, Zahara Michuzi ameipongeza GGML na wafanyakazi wanawake wanaofanya kazi katika kampuni hiyo kwa kuandaa mafunzo hayo yanayotoa mwangaza kwa wanafunzi wengi wa kike kujitambua na kufikia malengo sawa na viongozi wa kike waliofanikiwa katika nafasi mbalimbali.

“Binafsi sijafika hapa kwa nguvu zangu mwenyewe. Nilijitambua, nikamtanguliza Mungu lakini pia nikaomba watu mbalimbali akiwemo Profesa Peter Msofe wakati anafundisha Chuo Kikuu cha Dodoma kunipatia malezi ya kitaaluma ambayo yamenisaidia hadi kufikia hatua hii ya kuongoza Halmashauri ya Mji Geita kwa mafanikio,” alisema.

GGML imekuwa kinara wa uwekezaji kwenye jamii tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 ambapo vipaumbele vikuu vimekuwa ni miradi ya afya, elimu, maji, barabara, miradi ya kukuza kipato na miradi mingine mingi ya kijamii ili kuhakikisha jamii mwenyeji inapata maisha bora.

Kampuni imejenga zaidi ya shule saba za msingi na tano za sekondari ndani ya Mkoa wa Geita kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.

Mapema mwaka huu, GGML iliibuka mshindi wa jumla katika kampuni zinazofanya vizuri kwenye sekta ya madini nchini kwa mwaka 2020/2021 baada ya kunyakua tuzo katika vipengele vya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, mazingira, usalama, mlipaji bora wa kodi na uendelezaji wazawa.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button