Watakiwa kuzingatia sheria za ufugaji Musoma

Watakiwa kuzingatia sheria za ufugaji Musoma

Editha Majura, Musoma

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara, Bosco Ndunguru ameagiza wananchi kuzingatia sheria za ufugaji mijini, ili kunusuru mazingira hususan yanayozunguka miradi ya maendeleo.

Alitoa agizo hilo baada ya kukuta mifugo kwenye  majengo ya Shule mpya ya Sekondari ya Kigera, akawaomba wanaoishi jirani na miradi hiyo kuilinda.

Advertisement

“ Zipo sheria na taratibu zinazoelekeza jinsi ya kufuga mijini, ni lazima zifuatwe,” alisema.

Sekondari hiyo mpya inajengwa na Serikali kupitia Mpango wa Uboreshaji Elimu Sekondari (SEQUIP), ambapo Manispaa hiyo ilipokea Sh milioni 470 kati ya Sh milioni 600 inayotakiwa kukamilisha ujenzi huo.

Mbuzi wengi wameshuhudiwa wakiwa wamefungwa kamba na kubakizwa kwenye mazingira hayo, wengine wakizurura hovyo, huku vinyesi vyao vikiwa vimetapakaa mpaka ndani ya baadhi ya majengo ya shule hiyo.

Akizungumzia changamoto hiyo kwa njia ya Simu, Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Kigera, Jumanne Patrick, amesema elimu kwa umma kuhusu aina ya ufugaji unaotakiwa kufanyika mijini inatolewa kwa njia tofauti, lakini wafugaji wanakaidi.

“Siku chache zilizopita tulitembelewa na kamati ya kitengo cha ukaguzi cha manispaa. Moja ya mambo yaliyowaleta ni hili la kuzuia ufugaji katika maeneo ya wazi mjini, lakini wananchi wanakaidi,” amesema Patrick.

Kwa mujibu wake,  kabla ya ujio huo ulifanyika mkutano wa wakazi wa mtaa huo kwenye ofisi za Kata hiyo,  wananchi walihimizwa kutoachia mifugo au kuilisha kwenye maeneo ya wazi, lakini bado hawazingatii.

Amesema hatua iliyobakia ni kutumia sheria ndogo kudhibiti hali hiyo, ili mifugo inayokutwa ikirandaranda mitaani ikakamatwe na wahusika kuwajibishwa.