Wazazi washauriwa kufuatilia mwenendo wa watoto

WAZAZI wameshauriwa kufuatilia kwa karibu dalili zote za uchelewaji wa hatua za ukuaji wa lugha kwa watoto wao na kutafuta msaada wa kitaalamu wanapokuwa na mashaka na usikivu wa watoto.

Aidha, wamesisitiza kuweka juhudi katika mazoezi ya kuongea kwa watoto wenye changamoto ya usikivu ili maendeleo ya lugha yao yaendane na umri wao halisi. Hayo yameelezwa jana na Mtaalamu Mkuu wa Lugha katika Kliniki ya Usikivu ya HearWell Audiology, Rashida Hassuji wakati wa mafunzo ya siku mbili kwa wazazi wa watoto wenye tatizo la usikivu yaliyoandaliwa na Kliniki hiyo na kufanyika Dar es Salaam.

Rashida alisema kuwa”wazazi wanapaswa kufuatilia dalili zote za ucheleweshwaji wa hatua za ukuaji wa lugha na kutafuta msaada wa kitaalamu ikiwa wana mashaka.”

Advertisement

Mkurugenzi wa Kliniki ya HearWell ambaye ni mtaalamu bingwa wa usikivu, Fayaz Jaffer alisema kuwa wazazi wanatakiwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa urejeleaji wa watoto wao baada ya kuanza kusikia kupitia vifaa vya usikivu na vipandikizi.

Akizungmzia mafunzo ya wazazi wanayoyafanya kwa siku mbili na kwa wazazi 60, alisema kupitia mtaala ulioandaliwa na taasisi ya Med-EL ya Austria mahsusi kwa ajili ya wazazi utawawezesha kuwa sehemu ya safari ya maendeleo ya watoto wao kujifunza lugha na kuongea.

“Mtaala huu huwafundisha wazazi mbinu za kufanya mazoezi ya lugha nyumbani ili watoto wao waweze kuendeleza lugha na kuongea kwa haraka zaidi,” alifafanua.

Alieleza, kifaa cha usikivu, kinapopandikizwa kwa mtoto, huitaji mazoezi na mafunzo ya lugha kujua namna ya kuwasiliana na jamii na mzazi ndiye anayeweza kumjengea uwezo huo kwa urahisi na kwa haraka.

“Mtoto akishapandikizwa kifaa, ataweza kusikia milio mbalimbali bila kuelewa, hivyo huhitaji kufundishwa lugha ya usikivu kupitia akiwa na kifaa hicho, ndiyo maana tunasisistiza mafunzo haya,” alisema.

Kwa upande wake mzazi wa mtoto aliyepandikizwa vifaa vya usikivu Mariam Juma, alisema mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa nini cha kufanya kwa mtoto anayetumia vifaa hivyo ili aweze kuimarisha uwezo wake wa lugha.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *