Wenye ulemavu wanne wapata ajira

ARUSHA: VIJANA wanne wenye changamoto ya ulemavu mkoani Arusha wamepata ajira za kudumu katika kampuni ya RIJK ZWAAN, hatua inayodhihirisha kuwa watu wenye ulemavu wana uwezo wa kufanya kazi na kujitegemea wakipewa fursa na mazingira yanayowiana na uwezo wao.

Vijana hao, Willson Emmanuel, Vanesa Lucas, Dickson Francis na Eva Daud, wameajiriwa katika vituo viwili vya kampuni hiyo, Afrisem na Q-Sem, vilivyopo Tengeru na Usa River, vinavyojihusisha na uzalishaji, ukuzaji na uhimilishaji wa mbegu za mbogamboga.

Ajira hizo zimekuja baada ya vijana hao kupata huduma za urekebu na utengamao katika Kituo cha SIBUSISO, mkoani Arusha, ambapo walijengewa uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali za kuwawezesha kujitegemea.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mikataba ya ajira kwa vijana hao, Mkuu wa Programu wa SIBUSISO, Daniel Kirumba, alisema mpango wa kuwaunganisha vijana waliomaliza huduma kituoni na waajiri ulianzishwa baada ya kubaini kuwa baadhi yao hupoteza maendeleo waliyoyapata wanaporejea katika mazingira ya nyumbani.

Alisema awali kituo hicho hakikuwa na mpango maalumu wa kuwatafutia ajira vijana waliopitia huduma zake, lakini utafiti uliofanywa ulionesha umuhimu wa kuwaunganisha wale wanaoonesha uwezo wa kufanya kazi na fursa za ajira.

“Tumebaini kuwa vijana wengi wakirudi nyumbani maendeleo yao hushuka sana, licha ya kuwa wanakuwa wametoka hapa wakiwa wamepiga hatua kubwa. Ndiyo maana tukaamua kuanzisha programu ya kuwatafutia ajira wale wanaoonesha uwezo mkubwa wa utengamao na kufanya kazi,” alisema Kirumba.

Alisema ajira hizo si tu zitawasaidia vijana hao kujitegemea kiuchumi, bali pia zitabadilisha mtazamo wa jamii kuhusu watu wenye ulemavu kwa kuonesha kuwa wanaweza kushiriki katika uzalishaji na kuchangia maendeleo kama watu wengine.

Kirumba aliishukuru RIJK ZWAAN kwa kuwaamini vijana hao na kuwapa mikataba ya kudumu, akisema uamuzi huo ni mfano unaoweza kuigwa na waajiri wengine katika kutoa fursa kwa watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Kituo cha RIJK ZWAAN Q-Sem, Datius Bazima, alisema kampuni hiyo awali ilikuwa na mashaka kuhusu uwezo wa vijana hao kufanya kazi, lakini baada ya kuwapa nafasi walishangazwa na kiwango chao cha uchapakazi.

“Kweli wanapiga kazi hasa, sisi kama kampuni tunajiona kuwa tumetekeleza sera ya Serikali ya kutoa ajira kwa watu wenye ulemavu.

Wafanyakazi wenzetu wasio na ulemavu pia wamepokea vizuri jambo hili na kuona kuwa kumbe inawezekana,” alisema Bazima.

Alisema uzoefu wa kampuni hiyo umeonesha kuwa changamoto ya ulemavu si kikwazo cha mtu kufanya kazi, bali kinachohitajika ni kumpa nafasi, mazingira rafiki na majukumu yanayolingana na uwezo wake.

Ajira hizo pia zimeweka msingi wa SIBUSISO kuendelea kutafuta ushirikiano na waajiri mbalimbali ili kuwapa fursa vijana wengine wanaohitimu huduma za urekebu na utengamao katika kituo hicho.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button