Wilaya Tanganyika wapo kamili maandalizi kidato cha kwanza

Wanafunzi 3000 wanatarajia kuanza kidato cha kwanza Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, huku serikali ikisema maandalizi ya kuwapokea yamekamilika.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, Onesmo Buswelu akizungumza na wananchi katika ziara ya kukagua maandalizi ya kufungua shule katika Shule mpya ya Sekondari Majalila, Kijiji cha Majalila katika halmashauri hiyo.

Buswelu amewahimiza wazazi na walezi juu upatikanaji wa chakula pindi wanafunzi watakapokuwa shuleni, ili kuendelea kuwapatia ufanisi wawapo katika vipindi vya masomo.

Amesema wanafunzi walioandikishwa shule ya awali pamoja darasa la kwanza maandalizi pia yamekamilika kwa asilimia 99,  ambapo jumla ya vyumba vya madarasa 80 katika Wilaya hiyo vimekamilika sanjari na miundombinu yake pamoja na walimu.

Ametoa wito kwa walimu kuhakikisha wanahudhuria vipindi muda wote bila kukosa, ili shule hiyo mpya iweze kujinyakulia sifa nzuri ya kufaulisha na atakayebainika kushindwa kuhudhuria vipindi atachukuliwa hatua za kinidhamu.

“Kwa wale waliochaguliwa kujiunga kidato kwanza wahakikishe wote wanaripoti shuleni ifikapo Januari 9, 2023 siku ya Jumatatu,”amesema Buswelu.

Amesisitiza viongozi wa Serikali za mitaa kwa kushirikiana na viongozi wa dini, mila na wazazi kuhakikisha kila mtoto aliyefikia umri wa kwenda shule anaandikishwa na hasa wale wenye mahitaji maalum, ambao kwa mila baadhi wamezoea kuwaficha, hivyo alishauri wawatoe kwani miundombinu ya shule ni rafiki kwa wanafunzi wote.

Naye Ofisa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mwalimu Roza Nabahani amesema hakuna upungufu wa madarasa wala madawati, hivyo ametoa rai kwa wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao waliofaulu shule na sio kuwaozesha.

Habari Zifananazo

Back to top button