Wizara yafungua usajili tuzo za Serengeti 2026

DAR ES SALAAM :Wizara ya Maliasili na Utalii imetangaza rasmi  dirisha la usajili kwa wadau wa uhifadhi na utalii kuwania Serengeti Awards 2026, huku ikiwasisitiza kutumia fursa hiyo kuonyesha kazi, ubunifu na mafanikio yao katika uhifadhi wa wanyamapori, maliasili na uendelezaji wa utalii. Dirisha hilo litafunguliwa Agosti 20, 2026 na litafungwa Septemba 30, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Dk. Thereza Mugobi, amesema tuzo hizo zinafanyika kwa mara ya pili mwaka huu ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kutambua na kuthamini mchango wa wadau mbalimbali katika uhifadhi wa maliasili na urithi wa Taifa, pamoja na kukuza sekta ya utalii.

Amesema tuzo hizo pia zinalenga kutoa motisha kwa wadau kuendelea kuboresha utendaji wao na kuchangia katika kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoshindana katika soko la utalii duniani.

Dk. Mugobi amesema jumla ya vipengele 63 katika makundi saba zinatarajiwa kushindaniwa mwaka huu.

Makundi hayo ni Tuzo za Chaguo la Wananchi, Tuzo za Waendeshaji wa Utalii, Tuzo za Waongoza Watalii, Tuzo za Madaktari wa Wanyama, Tuzo za Huduma za Ukarimu, Tuzo za Uhifadhi, Tuzo za Elimu ya Utalii na Tuzo Maalumu za Kutambua Mchango.

Wadau wanaotarajiwa kushiriki ni pamoja na waendeshaji wa shughuli za utalii, waongoza watalii, watoa huduma za malazi na chakula, mashirika ya ndege, taasisi za utalii, vyombo vya habari, waandishi na wahamasishaji wa utalii, kampuni binafsi pamoja na wadau wengine wa uhifadhi na utalii.

Dk. Mugobi amesema wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania wanaruhusiwa kuwania tuzo hizo iwapo watatimiza vigezo na masharti yaliyowekwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Serengeti Awards, Hatibu Madudu, amesema mwaka huu kategoria zimeongezeka kutoka 56 za mwaka jana hadi 63, baada ya waandaaji kupokea maoni ya wadau na kufanya maboresho katika maeneo mbalimbali.

Amesema baadhi ya mabadiliko yalitokana na changamoto zilizobainika katika mchakato uliopita, ikiwemo idadi ya wateule au washindani katika baadhi ya kategoria.

Kwa mujibu wa Madudu, washiriki wamegawanywa katika makundi matatu, likiwemo la watoa huduma na watendaji katika sekta ya uhifadhi na utalii.

Madudu amesema wananchi watakuwa sehemu ya mchakato wa kuwapata washindi katika baadhi ya kategoria.

Akizungumzia suala la hali ya hewa, Dk. Mugobi amesema waandaaji watazingatia ratiba ya mvua itakayotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wakati wa kupanga ziara za wataalamu na Kamati ya Maandalizi katika maeneo ya washiriki.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha usalama wa wataalamu na kupunguza changamoto zinazoweza kusababishwa na mvua.

Hata hivyo, amesema mvua hazitazuia wadau kushiriki kwa kuwa usajili na upigaji kura utafanyika kwa njia ya mtandao.

Dk. Mugobi amesema watu wenye mahitaji maalumu pia wataruhusiwa kuwania tuzo hizo iwapo wanajihusisha na shughuli za uhifadhi au utalii na wanakidhi vigezo vya kategoria husika.

Amesema hatua hiyo inaendana na dhana ya utalii endelevu na jumuishi, unaozingatia ushirikishwaji wa makundi mbalimbali katika sekta ya utalii.

“Tunajali utalii endelevu ambao unazingatia makundi yote. Kwa hiyo watu wenye mahitaji maalumu pia wanaruhusiwa kuwania tuzo ikiwa wanajishughulisha na shughuli za uhifadhi au utalii na wanakidhi vigezo vya kategoria wanayowania,” amesema.

Dk. Thereza imewahakikishia wadau kuwa mchakato wa Serengeti Awards 2026 utasimamiwa kwa kuzingatia uwazi, usawa na uadilifu, huku taarifa za washiriki zikihakikiwa na utaratibu wa kushughulikia malalamiko ukizingatiwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button