Trust Fund kulinda hisa za wananchi

KAMPUNI ya TIB Rasilimali imeingia makubaliano ya ushirikiano na Kampuni ya Sheria ya Breakthrough Attorneys kwa ajili ya kusimamia mifuko ya amana (Trust Funds) na kutoa huduma za ushauri wa usimamizi wa mali.

Ushirikiano huo unalenga kuwezesha wananchi kulinda umiliki wa hisa zao kisheria na kuhakikisha zinarithishwa kwa vizazi vyao endapo mmiliki atafariki.Makubaliano hayo yalisainiwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TIB Rasilimali, Brighton Kinemo, pamoja na Mshirika Mkuu wa Breakthrough Attorneys, Vintan Mbwiro.

Akizungumza kabla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Kinemo alisema ushirikiano huo unaweka msingi wa kimkakati wa kuanzisha huduma za kitaalamu za usimamizi wa amana maalum kwa watu binafsi, familia, wafanyabiashara, wawekezaji, taasisi na mashirika mbalimbali.SOMA: BoT yaonya upotoshaji amana benki za biashara

Amesema uamuzi huo umetokana na kubaini kuwa wanahisa wengi wanapofariki dunia, hisa walizomiliki hukosa usimamizi mzuri na wakati mwingine hushindwa kuwanufaisha warithi wao kutokana na ukosefu wa mipango madhubuti ya urithi.”Kumekuwa na changamoto katika masuala ya urithi na wosia. Kupitia Mfuko wa Amana Maalum, hisa za mmiliki zitaweza kurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi, jambo litakalosaidia kuongeza utajiri wa familia na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa,” alisema Kinemo.

Amefafanua kuwa baba aliyenunua hisa akifariki dunia, watoto wake wataendelea kunufaika na mapato yatokanayo na hisa hizo, huku umiliki wake ukiendelea kubaki ndani ya ukoo kwa mujibu wa masharti ya amana.”Lengo ni kuhakikisha hisa hizo zinaendelea kumilikiwa na warithi wa familia na si kuuzwa ovyo kwa watu wengine, isipokuwa kwa mujibu wa masharti ya amana yaliyowekwa,” alisema.

Kinemo amesema huduma hiyo itasaidia familia kulinda mali na uwekezaji wao, kupanga urithi kwa utaratibu, pamoja na kuhakikisha biashara na mali zinaendelea kusimamiwa kwa uwajibikaji hata baada ya mwanzilishi kufariki.Amesema kadiri uchumi wa Tanzania unavyoendelea kukua, wananchi wengi wanazidi kumiliki mali, hisa, biashara na hati fungani, hivyo ni muhimu kuwepo mifumo madhubuti ya kusimamia mali hizo ili ziweze kupitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine bila migogoro.

Ameonya kuwa bila kuwa na mpango sahihi wa urithi, familia zinaweza kuingia kwenye migogoro, biashara kuyumba baada ya kuondokewa na waanzilishi wake, na warithi kushindwa kusimamia mali walizoachiwa. “Hapo ndipo umuhimu wa Mfuko wa Amana unapokuja. Ni huduma ya kisheria inayomwezesha mtu au taasisi kuweka mali zake chini ya usimamizi kwa manufaa ya warithi au walengwa wake kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa,” alisema.

Kwa upande wake, Mshirika Mkuu wa Breakthrough Attorneys Vintan Mbwiro, alisema kampuni hiyo imejipanga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma hiyo kupitia njia mbalimbali, ikiwemo vyombo vya habari na programu za uhamasishaji zitakazofika hadi vijijini. “Makubaliano haya ni muhimu kwa sababu tumebaini kuwa bado kuna pengo la uelewa wa masuala ya kisheria yanayohusu umiliki na urithishaji wa hisa, hati fungani na mali nyingine za uwekezaji. Tumejipanga kuhakikisha elimu hii inawafikia Watanzania wote,” alisema Mbwiro.

Habari Zifananazo

2 Comments

  1. I get paid more than $120 to $130 per hour for working online. I heard about this job 3 months ago and after joining this i have earned easily $15k from this without having online working skills.
    This is what I do…..    https://www.work27.info

  2. I get paid more than $120 to $130 per hour for working online. I heard about this job 3 months ago and after joining this i have earned easily $15k from this without having online working skills.
    This is what I do…..    https://www.work27.info

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button