Bendera ya Taifa ilinipa nguvu Scotland

MUOGELEAJI wa Tanzania, Collins Saliboko, amesema kuona bendera ya Taifa ikipepea kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola kulimpa hamasa kubwa ya kuendelea kupambana na kuboresha kiwango chake.
Akizungumza baada ya kurejea kutoka Scotland, muogeleaji huyo amesema moja ya vitu vilivyompa motisha zaidi ni kuona bendera ya Tanzania ikionekana katika uwanja wa mashindano, akisema ilikuwa fahari kubwa kuiwakilisha nchi.“Niliona bendera ya Tanzania ikionyeshwa kwenye screen na hiyo ilinipa nguvu zaidi ya kufanya vizuri. Ilikuwa jambo kubwa kwangu kujua kuwa ninaiwakilisha nchi yangu,” amesema.
Saliboko alishiriki mbio mbalimbali kuanzia mita 50 hadi mita 200 katika mashindano hayo, huku hivi karibuni akiandika rekodi yake bora ya msimu baada ya kumaliza mbio za mita 100 freestyle kwa wanaume kwa muda wa sekunde 53.10. Amesema bado anaamini ana nafasi kubwa ya kufikia hatua za juu zaidi katika mashindano makubwa baada ya kuona tofauti ya muda iliyopo si kubwa.
Amesema kwa sasa anataka kuweka mkazo zaidi katika maandalizi ya mbio za mita 50 huku akiendelea kuboresha muda wake kwenye mashindano mbalimbali yatakayofuata.SOMA: Mtanzania ang’ara kuogelea baharini Kenya
Saliboko aliwashukrani Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA) pamoja na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kwa msaada waliompa katika safari yake ya kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola 2026 iliyofanyika Glasgow, Scotland.



