Wanafunzi 95 waelekea India masomoni

DAR ES SALAAM: Wanafunzi zaidi ya 95 kutoka Tanzania wameondoka nchini kwenda India kwa ajili ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu katika vyuo mbalimbali, ikiwa ni kundi la kwanza kati ya wanafunzi 198 wanaotarajiwa kusafiri kwenda India kupitia Global Education Link mwaka 2026.

Wanafunzi hao wameondoka kupitia Kituo cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (Terminal 3) jijini Dar es Salaam, huku wengi wao wakichagua kusomea fani za sayansi, teknolojia na taaluma nyingine zinazokwenda sambamba na mahitaji ya uchumi wa dunia wa sasa.

Miongoni mwa fani wanazokwenda kusomea ni Uhandisi wa Kompyuta, Usalama wa Mtandao (Cyber Security), Akili Bandia (Artificial Intelligence), Uhandisi wa Ujenzi, taaluma mbalimbali za afya, Sheria na Usimamizi wa Biashara.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Meneja wa Tawi la Dar es Salaam wa kampuni hiyo, Micky Musa, alisema safari hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa kuwaunganisha vijana wa Tanzania na fursa za elimu ya kimataifa.

“Zaidi ya wanafunzi 95 wanaondoka katika kundi hili la kwanza kwenda India, huku kwa mwaka huu mzima tukitarajia jumla ya wanafunzi 198 kwenda kusoma nchini humo. Hili si kundi la mwisho, kwani bado tuna wanafunzi wengine wanaokamilisha taratibu zinazohitajika,” alisema Musa.

Aliongeza kuwa mbali na India, Global Education Link inaandaa kundi jingine la takribani wanafunzi 185 wanaotarajiwa kwenda China, huku wanafunzi wengine wakiwa katika hatua mbalimbali za maandalizi ya kwenda kusoma Malaysia, Marekani na Uingereza.

Musa aliwahimiza vijana wenye ndoto za kusoma nje ya nchi kutembelea ofisi za Global Education Link zilizopo Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mwanza na Arusha.

“Kadri muda unavyoendelea, Watanzania wataendelea kuona makundi zaidi ya wanafunzi yakiondoka kwenda kusoma nje ya nchi. Tunawahimiza vijana wanaotamani kusoma nje ya nchi kutembelea ofisi zetu. Bado kuna muda. Njooni na matokeo yenu ya masomo, Global Education Link iko tayari kusaidia kutimiza ndoto zenu,” alisema.

Aidha, Musa aliwahimiza wazazi na walezi ambao watoto wao wana nia ya kwenda kusoma nje ya nchi kutumia huduma za Global Education Link kwa ajili ya kupata mwongozo kuhusu uchaguzi wa vyuo na programu za masomo, udahili, taratibu za visa pamoja na maandalizi ya safari.

Miongoni mwa wanafunzi walioondoka ni wale wanaokwenda kusomea Computer Science, Artificial Intelligence na Cyber Security. Walisema wamechagua fani hizo kutokana na kasi ya maendeleo ya teknolojia na umuhimu unaoongezeka wa ujuzi wa kidijitali katika maendeleo ya uchumi wa kisasa.

Alvin Andrew Munda, mwenye umri wa miaka 17, anayekwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Lovely Professional University nchini India, alisema amechagua kusomea Computer Science kwa sababu analenga kujenga ujuzi wa vitendo katika teknolojia na baadaye kujikita katika taaluma ya Cyber Security.

Alisema msisitizo wa chuo hicho katika mafunzo ya vitendo na matumizi ya maabara ni miongoni mwa sababu zilizomfanya achague chuo hicho.

 

“Napendelea mfumo wa elimu unaoweka msisitizo zaidi kwenye mafunzo ya vitendo badala ya kuzingatia zaidi nadharia na mitihani. Nataka kutumia maarifa nitakayoyapata kutengeneza suluhisho na hatimaye kujikita katika Cyber Security, kwa sababu usalama wa mtandao una umuhimu mkubwa katika dunia ya sasa,” alisema.

Munda aliishukuru Global Education Link kwa msaada walioupata yeye na familia yake katika mchakato mzima, kuanzia uchaguzi wa chuo hadi maandalizi ya safari.

“Global imetuunga mkono katika mchakato mzima. Walituongoza katika kila hatua na kuwa kiungo kati yetu, wazazi wetu na chuo hadi kufikia hatua hii ya kuwa uwanja wa ndege tayari kwa safari,” alisema.

Mwanafunzi mwingine anayekwenda kusomea fani zinazohusiana na Computer Science na Artificial Intelligence alisema anatarajia kuwa mtaalamu wa data na teknolojia katika miaka ijayo.

Alisema Artificial Intelligence tayari imekuwa sehemu muhimu katika sekta za benki, afya, biashara, serikali na sekta nyingine, hivyo elimu katika eneo hilo itamwezesha kushiriki katika maendeleo ya teknolojia nchini Tanzania.

Aidha, mwanafunzi mwingine anayekwenda kusomea Shahada ya Usimamizi wa Biashara pamoja na Shahada ya Sheria (Bachelor of Business Administration and Bachelor of Laws) alisema anatamani kuwa mwanasheria na mjasiriamali mwenye mafanikio baada ya kukamilisha masomo yake.

Alisema Global Education Link imekuwa na mchango mkubwa katika kumwezesha kufikia hatua ya kwenda kusoma nje ya nchi.

“Global Education imetusaidia sana, hasa katika mchakato wa visa, kupangiwa chuo na maandalizi mengine ya safari. Ushirikiano kati yangu, wazazi wangu na Global Education umetufikisha hapa tulipo leo,” alisema.

Kwa upande wao, wazazi waliowasindikiza watoto wao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere waliipongeza Global Education Link kwa kusimamia maandalizi ya wanafunzi kuanzia hatua za awali hadi siku ya kuondoka.

Donald Kito, mzazi wa Isaac Donald Kito, ambaye anaelekea Lovely Professional University kusomea Diploma ya Uhandisi wa Ujenzi, alisema familia yao ilifahamu kuhusu Global Education Link kupitia matangazo.

Alisema baada ya kuwasiliana na taasisi hiyo, walipatiwa taarifa na mwongozo wa kina uliowapa ujasiri wa kuendelea na mchakato wa kumpatia mtoto wao nafasi ya kusoma nje ya nchi.

Kuondoka kwa wanafunzi hao kunaonesha kuongezeka kwa hamu miongoni mwa vijana wa Tanzania ya kupata elimu na sifa za kitaaluma zinazotambulika kimataifa, hususan katika nyanja za teknolojia, uhandisi, biashara, sheria na taaluma nyingine zinazoendana na mahitaji yanayobadilika ya uchumi wa dunia.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button