Vikundi vya wajasiriamali 33,594 vyanufaika mikopo asilimia 10

DODOMA; Serikali imesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25 hadi 2025/26 jumla ya vikundi vya wajasiriamali 33,594 vilinufaika na mikopo ya asilimia 10 na  kiasi cha shilingi bilioni 357.20 kilikopeshwa kwa vikundi hivyo.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Septemba 4, 2026 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Festo Dugange alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Chiku Athman Issa, aliyehoji serikali haioni sababu kubwa ya kutokuwa na matokeo makubwa ya mikopo ya asilimia 10, tangu ianze ni kukosekana wataalam wa mafunzo ya biashara.

Amesema kati ya vikundi vilivyopata mkopo vikundi vya wanawake 18,539, vikundi vya vijana 11,758 na vikundi vya watu wenye ulemavu 3,247.

“Kiasi cha shilingi bilioni 357.20 zilikopeshwa kwa vikundi hivyo, aidha,  kati ya fedha hizo, kiasi cha  Shilingi bilioni 143.43 zilikuwa zimefikia muda wa marejesho na kati ya kiasi hicho, Shilingi bilioni 130.04, sawa na asilimia 91 zimerejeshwa,” amesema.

Amesema katika utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wajasiriamali serikali imeweka mwongozo wa kuwatumia wataalamu wa fedha, maendeleo ya jamii na wataalamu wengine walioko katika halmashauri kuwaelimisha, kuwasimamia wajasiriamali wanaoomba mikopo.

“Aidha, mwongozo huo umeweka utaratibu wa kutoa mafunzo ya masuala ya fedha na ujasiriamali kwa vikundi vinavyoomba mikopo ili kuwazesha kunufaika na mikopo hiyo.

“Serikali itaendelea kuboresha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wajasiriamali kwa kuwatumia wataalamu wa mafunzo ya biashara ili kuongeza ufanisi wa mikopo hiyo,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button