Mwenge wafungua fursa za vijana Kyerwa

KYERWA: Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Michael Mwango’nda, ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa kuhakikisha majukwaa ya vijana yanashushwa kutoka ngazi ya wilaya hadi kata, vijiji na mitaa, ili vijana wengi zaidi waweze kupata elimu na taarifa kuhusu fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali.

Mwango’nda alitoa agizo hilo wakati akizindua Jukwaa la Vijana katika Wilaya ya Kyerwa, mkoani Kagera, akisema majukwaa hayo yakifikishwa katika maeneo wanayoishi vijana yatawezesha wengi kupata elimu kuhusu fursa za kiuchumi, ikiwemo mikopo.

Alisema Serikali imeweka nguvu kubwa katika kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia vikundi mbalimbali, hivyo viongozi na watendaji wa Halmashauri wanapaswa kuongeza juhudi za kuwafikia vijana katika maeneo yao.

“Serikali imeweka nguvu nyingi kwa vijana na hamasa ya sasa ni kuhakikisha vijana wanajiajiri kupitia vikundi mbalimbali. Serikali iko tayari kuwahangaikia; kinachopungua kwa sasa ni elimu na namna ya kutumia fursa zilizopo. Hivyo viongozi wa Halmashauri wanapaswa kujiongeza na kuwafikia huko huko walipo,” alisema Mwango’nda.

Kwa upande wake, Afisa Vijana wa Wilaya ya Kyerwa alisema katika Kongamano la Vijana kuwa hadi sasa jumla ya vijana 1,244 kutoka kata 24 za wilaya hiyo wamefikiwa na fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri.

Alisema upatikanaji wa mikopo hiyo umeongeza fursa kwa vijana kupanua mitaji ya biashara na shughuli zao za kiuchumi, hatua inayochangia kuinua kipato na uchumi wa familia zao.

Katika ziara yake ya Mbio za Mwenge wa Uhuru, Mwango’nda pia alizindua mradi wa kikundi cha vijana cha Umoja wa Mafundi Nyamiyaga, ambacho kimenufaika na mkopo wa Sh milioni 61.

Mwenyekiti wa kikundi hicho, Yusto Rutahananwa, alisema Serikali pia imewaunga mkono kwa kuwapatia mashine za kuchomelea zenye thamani ya Sh milioni 1.5, zitakazowawezesha kuongeza uzalishaji na kipato.

Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Zaitun Msofe, alisema Halmashauri itaendelea kutoa elimu kwa vijana kuhusu fursa zinazotolewa na Serikali na kuhakikisha huduma hizo zinawafikia vijana hadi ngazi ya vijiji.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button