Wizara ya Katiba na Sheria yapitia sheria kulinda uwekezaji

DAR ES SALAAM: WIZARA ya Katiba na Sheria imeanza kupitia sheria mbalimbali za kisekta nchini ili kuhakikisha zinaendana na mahitaji ya sasa pamoja na malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ili kuweka mfumo imara wa kisheria utakaowezesha utekelezaji wa shughuli za kiuchumi, ikiwemo uwekezaji katika sekta ya Uchumi wa Buluu, huku ukilinda maslahi ya taifa na kuimarisha mazingira ya uwekezaji.

Akizungumza leo, Septemba 7, 2026, katika Kongamano la Tano la Kimataifa la Uchumi wa Buluu linalofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, Wakili Mkuu wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Richard Jacopiyo, amesema sheria ni nyenzo muhimu katika kuweka mazingira bora na wezeshi kwa uwekezaji.

Jacopiyo amesema Tanzania haiwezi kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 bila kuwa na mfumo wa kisheria unaoendana na mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia.

Amesema mapitio hayo yatahusisha sheria za sekta mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha zinaendana na mwelekeo wa taifa na kuchangia katika kukuza uchumi, kuongeza pato la taifa na kuimarisha maendeleo ya kijamii.

“Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka mikakati madhubuti ya kufikia maendeleo yaliyokusudiwa. Kwa hiyo, sheria zinapaswa kuwa sehemu ya msingi katika kuhakikisha malengo hayo yanatekelezwa kwa ufanisi,” amesema Jacopiyo.

Katika hatua nyingine, Wizara hiyo imewataka wawekezaji na wadau wa Uchumi wa Buluu kutumia njia mbadala za utatuzi wa migogoro pale inapotokea migogoro kati ya wawekezaji na watoa huduma.

Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Daniel Mbaki, amesema kuongezeka kwa shughuli za uwekezaji katika Uchumi wa Buluu kunaweza kuongeza uwezekano wa kutokea kwa migogoro kati ya wawekezaji na wadau mbalimbali.

Amesema Wizara inahamasisha matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro, ikiwemo upatanishi, usuluhishi na majadiliano, ili kuwawezesha wahusika kupata suluhu kwa ufanisi bila kupitia taratibu ndefu za utatuzi wa migogoro.

Mbaki amesema kupitia kitengo maalum cha utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, Wizara imekuwa ikisajili wataalamu wanaotoa huduma hizo, wakiwemo wapatanishi, wasuluhishi na wawezeshaji wa majadiliano.

Aidha, amewataka watu wanaotaka kutoa huduma za utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala kujisajili kupitia mfumo wa NARIS, unaopatikana mtandaoni na kuwawezesha waombaji kufuata taratibu zote zinazohitajika.

Mbaki amesema wadau wanaohitaji maelekezo zaidi kuhusu usajili na huduma za utatuzi wa migogoro wanaweza kutembelea banda la Wizara katika kongamano hilo kwa ajili ya kupata elimu na ufafanuzi zaidi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button