Sh milioni 91.1 kusogeza maji Kilimahewa

MTWARA: WAKAZI wa Kijiji cha Kilimahewa Kata ya Mnongodi Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara wameishukuru serikali kwa kuwaletea huduma ya maji kwenye kijiji hicho mradi uliyogharimu Sh milioni 91.1
Wakizungumza kwenye halmashauri hiyo katika kijiji hicho cha kilimahewa akiwemo Shani Athumani amesema kwa sasa wakazi hao hawana changamoto ya maji ikilinganishwa na hapo awali .
Hayo yamejiri leo Septemba 10, 2026 wakati Mbunge wa Jimbo la Nanyamba mkoani humo Abdallah Chikota alipozungumza wa wakazi hao kupitia mkutano wa hadhara wenye lengo la kuwashukuru kwa kuendelea kukiunga mkono Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Sambamba na hilo kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua ili kupata maendeleo endelevu.
Amesema huduma hiyo kwa sasa inapatikana kwa uhakika katika mradi wa maji kilimahewa ikiwa hapo awali walikuwa wanapata maji eneo la bonde lililopo kwenye kijiji hicho ambapo siyo salama kwa afya zao.
“Kitendo cha serikali kutuletea maji karibu hapa kijijini kwetu ni jambo kubwa sana kwetu kwasababu tumeondokana na kero hii ya maji iliyokuwa inatukabili,”amesema Shani
Mkazi mwingine wa kijiji hicho ni Juma Maulidi pamoja na shukrani hizo ameiomba serikali kuwapunguzia gharama ya maji hayo ambayo bei ni Sh 100 kwa dumu moja la rita 20 na badala yake iwe Sh 50 kwa dumu hilo ikilinganishwa na kupanda kwa gharama ya maisha kwa sasa.

Kwa upande wake mbunge huyo, amesema serikali ipo kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kijamii kwa urahisi kwenye maeneo yao ikiwemo hiyo ya maji.
Aidha amesisitiza suala la utunzaji wa miradi hiyo ya maendeleo ambayo serikali inawekeza fedha nyingi ili kumrahisishia mwananchi upatikanaji wa huduma hizo muhimu za kijamii.



