TRA yamfikia mfanyabiashara baada ya janga la moto

DODOMA: Uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dodoma, kupitia Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara, umemtembelea mfanyabiashara, Amedius Michael, aliyekumbwa na janga la moto lililoathiri ghala lake la biashara la AM Shopping Center.

Ziara hiyo iliyoongozwa na Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma,  Pendolake Elinisafi, imelenga kumpa pole na kumfariji mfanyabiashara huyo, pamoja na kutathmini athari za janga hilo katika shughuli zake za biashara.

Aidha, ziara hiyo imelenga kubaini namna Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara linavyoweza kumsaidia mfanyabiashara huyo katika kurejesha shughuli zake baada ya kupata hasara kutokana na tukio hilo.

Ghala hilo lilikuwa likihifadhi bidhaa mbalimbali za plastiki pamoja na bidhaa za umeme, ambazo ziliathiriwa na kuteketea kufuatia janga hilo la moto.

Kupitia ziara hiyo, TRA Dodoma imeendelea kuonesha ukaribu wake na walipakodi, ikiwemo kuwafikia na kuwapa ushauri wakati wanapokumbwa na changamoto zinazoweza kuathiri shughuli zao za kiuchumi.

Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara linaendelea kufanya kazi bega kwa bega na walipakodi kwa kuwapatia elimu, ushauri na uwezeshaji unaolenga kuwasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali za biashara na kuimarisha shughuli zao.

TRA Dodoma imesisitiza dhamira yake ya kuwa karibu na walipakodi na kuhakikisha wanapata huduma, elimu na ushauri unaostahili ili biashara zao ziweze kurejea katika hali ya kawaida, kukua na hatimaye kuchangia katika ukuaji wa uchumi na mapato ya Serikali.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button