Sendiga awaonya wanaochochea migogoro

MOROGORO: Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Sendiga, amesema atachukua hatua dhidi ya baadhi ya viongozi wa vijiji wanaodaiwa kuwa vyanzo vya kuchochea migogoro baina ya wakulima na wafugaji katika maeneo yao.
Sendiga amesema hayo Septemba 17, 2026, wakati wa kikao chake cha kwanza na waandishi wa habari tangu alipokabidhiwa rasmi majukumu ya uongozi wa mkoa huo, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo katika jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kutatua migogoro baina ya wakulima na wafugaji, ikiwa ni pamoja na kuanza kwa zoezi la utambuzi wa mifugo na wafugaji kwa lengo la kuimarisha amani na utulivu kwa wananchi.
“Hakuna ng’ombe wanaingia kijijini kama hakuna mtu anayefahamu. Tunajua kuna baadhi ya vijiji na baadhi ya viongozi wa vijiji ambao wanafahamu leo mfugaji gani anaingiza mifugo,” amesema Sendiga.

Amesema viongozi hao wanafahamika na kwamba Serikali kupitia wakuu wa wilaya pamoja na vyombo vya dola inawafahamu, hivyo amewataka kuacha vitendo vinavyoweza kuchochea migogoro katika maeneo yao.
“Tunawajua, na waheshimiwa wakuu wa wilaya wanawajua na vyombo vinawajua. Sasa wakae mkao wa kula, huwezi ukapata wewe raha, usumbue nchi, haiwezekani. Tunakwenda kusumbuana huko huko,” ameonya Sendiga.



