Bil 3/-kutumika upanuzi mtandao maji Nyang’hwale

SERIKALI imetenga Sh bilioni 3.86 kupitia Mfuko wa Lipa kwa Matokeo (PforR) kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji toka Nyamtukuza kwenda vijiji vya Bululu, Ifugandi na Busolwa wilayani Nyang’hwale mkoa wa Geita.
Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) wilayani Nyang’hwale Moses Mwampunga amesema hayo wakati akitoa taarifa ya mradi kwa viongozi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka 2024.

Amesema tayari Sh bilioni 3.83 zimeshatumika huku jamii ikichangia ardhi kwenye maeneo yalipopita mabomba ya maji na miundombinu ya maji kujengwa.
SOMA: Kiongozi Mbio za Mwenge awafagilia RUWASA Mtwara
Moses amesema mradi huo umefikia asilimia 95 ya ujenzi hadi sasa na hadi kukamilika RUWASA inategemea kupata maji kutoka katika bomba linalotoa maji Kijiji cha Mhangu (Shinyanga) hadi Ilogi (Kahama).
“Mradi huu una bomba kuu umbali wa mita 15,815 na utahudumia vijijiji vitatu vyenye jumla ya wakazi wapatao 20,402,” amesema Moses.

Amesema upanuzi wa mtandao wa maji utawezesha wananchi kupata maji safi na salama, kupunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu unaozidi mita 400 na kupunguza magonjwa yanayosababishwa na maji yasiyo salama.
Hadi Septemba 2024 wilaya ya Nyang’hwale imefanikiwa kufikisha huduma ya maji safi na salama katika vijiji 47 sawa na asilimia 75 ya vijiji vyote 62 wilayani humo.

Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale, Iddi Kassu amesema huo ni mwendelezo wa serikali kusogeza huduma za maji kwenye maeneo yote ili kuondoa adha itokanayo na ukosefu wa maji safi na salama.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2024, Godfrey Mzava ameweka jiwe la msingi katika mradi huo huku akiwataka RUWASA kutekeleza miradi kwa wakati ili kufikia malengo ya serikali kama ilivyopangwa.



